Na Avelina Musa - Dodoma.
IMEELEZWA kuwa katika kipindi cha Uongozi wa Serikali ya awamu ya sita hali ya Uchumi ya Mkoa wa Geita imeendelea kuimarika ambapo Pato halisi lilikua kutoka Shilingi 7,031,590,000/= mwaka 2021 hadi Shilingi 9,122,637,000 mwaka 2024 sawa na ukuaji wa asilimia 31 ambapo pato la mtu mmoja limeongezeka kutoka shilingi 2,769,308/= mwaka 2021 hadi shilingi 2,814,714/= mwaka 2024 sawa na ongezeko la asilimia 1.6.
Hayo yameelezwa na Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhe.Martine Shigela wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Sita leoJulai 21 2025 Jijini Dodoma ambapo amesema Serikali imeendelea kutilia mkazo umuhimu wa maendeleo kwa wananchi pamoja na ushirikishwaji wa makundi maalum ikiwemo vijana, wanawake na Watu Wenye Ulemavu ili kuleta usawa wa kijamii na kiuchumi kwa wote.
Amesema katika kipindi cha miaka minne ya serikali ya awamu ya sita Mkoa umepata Mafanikio mengi ambapo katika sekta ya Afya miundombinu ya kutolea huduma za afya imeboreshwa na kuongezeka kwa upatikanaji wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi na kuimarika kwa upatikanaji wa huduma za afya karibu na wananchi.
Mhe.Shigela amesema mafanikio hayo ni pamoja na Kukamilika kwa ujenzi wa Hospitali za Halmashauri za Bukombe, Chato, Geita, Geita Manispaa, Mbogwe na Nyang’hwale;Kukamilika kwa ujenzi wa majengo matatu (3) ya huduma za dharura (EMD) katika Hospitali ya Bukombe, Katoro na Hospitali ya Halmashauri Nyang’hwale;Kukamilika kwa ujenzi wa jengo la wagonjwa mahututi katika Hospitali ya Halmashauri ya Geita (Nzera) na ukarabati wa Hospitari ya Halmashauri ya Bukombe na Manispaa ya Geita;Kuongezeka kwa idadi ya zahanati kutoka 129 mwaka 2021 hadi 198 mwaka 2025
" Kuongezeka kwa vituo vya afya kutoka 25 mwaka 2021 hadi 42 mwaka 2025; Kuongezeka kwa nyumba za watumishi wa afya kutoka 180 mwaka 2021 hadi 230 mwaka 2025; Kuongezeka kwa upatikanaji wa dawa, vifaa, vifaa tiba na vitendanishi katika vituo vya kutolea huduma za afya kutoka asilimia 80 mwaka 2021 hadi asilimia 90 mwaka 2025;Kupunguza vifo vya mama wajawazito kutoka 57 mwaka 2021 hadi vifo 55 mwaka 2025; naKupunguza maambukizi ya Virusi vya UKIMWI kutoka 5.1% mwaka 2021 hadi kufikia 4.90% mwaka 2025."Amesema.
Aidha amesema Mafanikio yaliyopatikana katika sekta ya elimu yamewezesha kuongezeka kwa uandikishaji na udahili wa wanafunzi, ufaulu pamoja na kupunguza umbali wa wanafunzi kufuata huduma ya elimu. Mafanikio hayo ni pamoja na:Kuendelea kutekeleza Mpango wa Elimu bila Ada kuanzia elimu ya awali hadi kidato cha sita kwa kuongeza fedha za kugharamia mpango huo kutoka Shilingi 6,486,387,724.00/= mwaka 2021 hadi Shilingi 19,989,544,192/=mwaka 2025
"Katika kipindi cha kuanzia mwaka 2021 hadi 2025 Serikali ya awamu ya sita iliweka kipaumbele cha kuendelea kuimarisha upatikanaji wa huduma ya maji kwa wananchi ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kaya nyingi zaidi zinaunganishwa na huduma ya maji."Amesema.
Serikali ya awamu ya sita imeendelea kutekeleza shughuli za kilimo katika Mkoa wa Geita kwa kuhakikisha kilimo kinakuwa chenye tija na usalama wa chakula unaimarika.
Amesema Serikali ya awamu ya sita chini ya usimamizi wa Chama Cha Mapinduzi inatambua umuhimu wa sekta ndogo ya Mifugo kama shughuli kuu ya kiuchumi kwa wakazi wa Mkoa. Kutokana na umuhimu huo, Serikali ya Mkoa wa Geita katika kipindi cha kuanzia mwaka 2021 had 2025 imeendelea kuhimiza ufugaji wa kisasa wenye kuzingatia kinga, tiba na utafiti wa mifugo ili ufugaji uweze kuwanufaisha wananchi.
Hata hivyo amesema Sekta ya nishati imeendelea kuwa mhimili muhimu katika kuwezesha utekelezaji wa shughuli za kiuchumi na kijamii katika Mkoa wa Geita. Kutokana na hilo, CCM iliisimamia Serikali katika kuhakikisha kuwa Mkoa unakuwa na nishati ya kutosha ili kukidhi mahitaji ya kiuchumi na kijamii.
Serikali inatambua kuwa sekta ya michezo na sanaa ina umuhimu mkubwa katika kutoa burudani, kuelimisha jamii, kuimarisha afya, kuunganisha jamii, kuzalisha ajira na kudumisha mila, tamaduni na desturi za kitanzania.


