Na Jackline Minja WMJJWM
Musoma – Mara
Serikali imesisitiza umuhimu wa jamii kuimarisha maadili na uzalendo miongoni mwa vijana nchini kwa kutumia taasisi za elimu ili kujenga taifa lenye misingi imara ya utu, uwajibikaji.
Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Mhandisi Maryprisca Mahundi, akiwa mgeni rasmi katika Mdahalo wa maadili na uzalendo uliofanyika katika Chuo cha Maendeleo ya Jamii Buhare, mkoani Mara.
Mhe. Mahundi amesema, Serikali ya Awamu ya Sita inaamini kuwa maendeleo ya kweli ya taifa hayawezi kupatikana bila kujenga maadili ya wananchi wake, hususan vijana ambao ndiyo nguvu kazi na viongozi wa baadaye.
“Huwezi kujenga taifa lenye maendeleo ya kweli bila kujenga maadili ya raia wake. Vijana wanapaswa kulelewa katika misingi ya utu, uzalendo, uwajibikaji na kuheshimu sheria, kwa sababu wao ndiyo nguzo ya sasa na ya baadaye ya taifa letu, vyuo vina nafasi ya kipekee katika kumjenga kijana kwa sababu vinamgusa katika hatua muhimu ya maisha yake hivyo serikali itaendelea kushirikiana na vyuo ili kuhakikisha elimu ya maadili na uzalendo inakuwa sehemu ya kudumu ya mifumo ya malezi” alisema Mhe. Maryprisca.
Awali, Mkuu wa Chuo cha Maendeleo ya Jamii Buhare Paschal Mahinyila amesema, mdahalo huo ni utekelezaji wa maelekezo ya Wizara, lakini pia ni sehemu ya dhamira ya Chuo katika kuwajenga wanachuo kuwa raia wenye maadili na uzalendo. Chuo hicho kimejikita katika malezi ya wanachuo kwa kuzingatia maeneo matatu muhimu ya ukuaji wa binadamu ambayo ni akili, roho na haiba, huku akisisitiza kuwa malezi hayo ndiyo msingi wa kujenga raia bora.
“Mdahalo huu ni utekelezaji wa maelekezo ya Wizara yetu, lakini pia ni sehemu ya mkakati wa Chuo wa kuwajenga vijana wenye maadili mema, uzalendo wa dhati na uwajibikaji kwa taifa lao, tunaamini kuwa huwezi kumlea binadamu kamili bila kuzingatia ukuaji wa akili, roho na haiba. Ndiyo maana Chuo kimeweka mifumo ya kufundisha uraia, kuhimiza nidhamu, maadili, mavazi rasmi na kutoa fursa za malezi ya kiroho kwa wanachuo,” alisema Mkuu wa Chuo.
Nao baadhi ya washiriki wa mdahalo huo wakiwemo wanachuo, viongozi wa dini na wananchi wanaoizunguka chuo, wameipongeza Serikali kwa kuendelea kuwekeza katika mijadala ya kujenga maadili na uzalendo, wakisema kuwa hatua hiyo inachangia kwa kiasi kikubwa kubadilisha mitazamo ya vijana.
Aidha, Washiriki hao wamesisitiza kuwa, kuendelezwa kwa midahalo ya aina hiyo kutasaidia kujenga jamii yenye mshikamano, uwajibikaji na heshima kwa tunu za taifa, huku wakitoa wito kwa viongozi wengine kuiga mfano huo wa kuwafikia wananchi moja kwa moja.

