Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule ameuelekeza uongozi wa Shule ya Sekondari Chilonwa iliyopo Wilayani Chamwino kuhakikisha wanakamilisha Majengo yaliyobainika kuwa na dosari kwa wakati ikiwa ni ujenzi wa miundombinu ya maboma 8 ya madarasa, mabweni 4 na matundu ya vyoo 13 kwa ajili ya wanafunzi wa kidato cha tano wanaotarajiwa kuanza masomo ifikiapo agosti 14 Mwaka huu.
Mhe. Senyamule amebainisha hayo leo Julai 20, 2023 wakati wa ziara yake ya kikazi katika Shule hiyo kwa lengo la ukaguzi wa miundombinu mbalimbali kama sehemu ya maandalizi ya kupokea wanafunzi wa kidato cha tano.
Ameelekeza miradi hiyo kukamilika kwa wakati na ubora utakaoendana na thamani ya fedha zilizotolewa ili wanafunzi wa kidato cha tano watakapowasili yawe tayari kutumika na mpaka sasa imefikia hatua za ukamilishaji ikiwa vyumba 8 vya madarasa vimefikia asilimia 99, mabweni asililimia 85% na matundu ya vyoo asilimia 99.5 sambamba na madawati na viti kwa wanafunzi 400, vitanda 70 kati ya 120 vimekamilika.
Awamu ya kwanza shule hiyo ilipokea kiasi cha zaidi ya shilingi milioni 581 na awamu ya pili kiasi cha shilingi milioni 125 kwa ajili ya Ujenzi wa bweni moja. "Hakikisheni mnaongeza wasaidizi kwa ajili ya kuongeza nguvu kazi na muda ikiwezekana hadi usiku bahati nzuri hapa kuna umeme hivo kazi zifanyike usiku na mchana na kwa unadhifu ili tukamilishe kwa ajili ya wanafunzi wetu wa kidato cha tano", amesisitiza.Mhe. Senyamule.
Pia, Mkuu wa Mkoa huyo baada ya ziara yake alishiriki hafla ya kupokea vifaa vya samani walizopewa kutoka Bank ya NMB vyenye Jumla ya thamani ya zaidi ya shilingi milioni 43 ikiwa ni sehemu ya kurudisha shukrani kwa jamii.
Benki ya NMB kama sekta binafsi nchini imeendelea kuunga mkono jitihada za Serikali katika sekta ya Afya na Elimu, kwa kuchangia samani mbalimbali pamoja na Mabati 188 kwa ajili ya kusaidia uezekaji katika Shule ya Sekondari Makangwa, Mabati 111 na vifaa vingine vya uezekaji kwa ajili ya shule ya msingi Mizengo Pinda ,Mabati 95 na vifaa vingine vya uezekaji kwa ajili ya shule ya msingi Chinangali.
Vifaa vinginine ni pamoja na Mabati 160 na vifaa vingine vya uezekaji kwa ajili ya shule ya msingi Dabaalo, Viti na Meza 50 kwa ajili ya Shule ya Sekondari Ntyuka, Mabenchi 30 ya kukalia wagonjwa katika Hospitali na Stuli 60 na makabati ya maabara kwaajili ya shule ya sekondari Buigiri vyenye Jumla ya thamani ya zaidi ya shilingi milioni 43 ambapo vifaa hivyo vimekabidhiwa na Meneja wa Kanda ya kati ya Benki hiyo Bi.Janeth Shango.
Kwa Upande Wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Chamwino Dkt. Semistatus Mashimba ameahidi ushirikiano katika kuhakikisha samani walizopewa na NBC zinatunzwa na kutumika kwa matumizi yaliyokusudiwa.
Naye, Diwani wa Kata ya Buigiri Mhe. Kenneth Yindi amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuboresha sekta ya Elimu kwa miundombinu wezeshi kwa wanafunzi kuweza kujifunza maarifa ili kuongeza watu wataalamu kwa ajili ya taifa la kesho
Aidha Mhe. Senyamule amewapongeza Walimu na Wanafunzi wa Shule hiyo kwa Matokeo mazuri ya ufaulu wa alama daraja la kwanza na pili matokeo ya kidato cha Sita mwaka huu.