VYANZO VIPYA VYA UMEME KUANZISHWA KUKIDHI ONGEZEKO LA MAHITAJI
Ijumaa, Februari 09, 2024
0
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amesemaSerikali imeamua kutekeleza miradi mipya uzalishaji wa umeme badala ya
kutegemea vyanzo vya zamani ili kuendana ongezeko kubwa la mahitaji ya
umeme nchini.
Dkt. Biteko amesema hayo tarehe 08 Februari 2024 Jijini Dodoma wakati
baada ya kushuhudia utiaji saini mkataba wa ujenzi wa mradi wa
uzalishaji umeme wa megawati 49.5 kwa nguvu ya maji katika Mto
Malagarasi mkoani Kigoma. Mkataba huo umesainiwa na Shirika la Umeme
nchini (TANESCO) na kampuni ya Dongfang Electric International kutoka
Jamhuri ya Watu wa China.
“Lazima tuwe na vyanzo vingi na vipya vya umeme, kiu na njaa ya umeme
tuliyonayo inatufanya tufikirie namna ya kupata umeme kwa haraka,
mahitaji ya umeme yameongezeka sana lakini vyanzo ni vilevile kwa
miaka mingi mfano Bwawa la Mtera lilijengwa mwaka 1980, Kidatu mwaka
1975, Kihansi mwaka 2000, Pangani 1995, Hale 1968, Nyumba ya Mungu
1964 na mwaka 2019 baada ya Gesi kuanza uzalishaji umeme mahitaji
yalikuwa pungufu kuliko uzalishaji, lakini sasa mahitaji ni makubwa
kuliko vyanzo.” Amesema Dkt. Biteko
Amesema kutokana na mahitaji ya umeme kuwa makubwa kuliko vyanzo
vyake, Serikali inaendelea kuongeza vyanzo vipya ikiwemo mradi wa
Malagarasi ambao utekelezaji wake utachukua miezi 42 na utekelezaji wa
mradi wa Julius Nyerere (JNHPP) ambao kwa sasa umekamilika kwa
asilimia 96 na unatarajia kuingiza umeme kwenye gridi ya Taifa mwezi
huu.
Ameeleza kuwa, utekelezaji wa miradi hiyo mipya ni maagizo ya Rais,
Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwa vyanzo vyote vilivyopo vianze kujengwa
sasa ukiwemo miradi ya umeme ya Kakono, Kikonge, Luhudji, Rumakali na
miradi ya Gesi mkoani Mtwara ili kuwa na umeme wa kutosha kwa mahitaji
ya nchi.
Ili kuwa na umeme kutoka vyanzo mchanganyiko, Dkt, Biteko
ametanabaisha kuwa, ameshatoa maagizo kwa watendaji wa Wizara na
TANESCO kuhakikisha wanabadilika na kuboresha huduma zao kwa wananchi
na kuwezesha uwekezaji katika miradi ya kuzalisha umeme kwa nguvu ya
Jua na Upepo.
Akizungumzia hali ya umeme Mkoani Kigoma, Dkt. Biteko amesema Pamoja
na mradi wa Mto Malagarasi, kuna miradi mingine mitatu ikiwemo
usafirishaji wa umeme kutoka Nyakanazi hadi Kigoma (kV 400), Tabora
hadi Kigoma (kV 132), kuongezwa uwezo wa kituo cha umeme wa Jua cha
Kigoma kutoka megawati 5 hadi megawati 10
Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko amesema kuwa uboreshaji wa
miundombinu nchi nzima unaendelea na hii inajumuisha ujenzi wa vituo
vya kupoza umeme katika maeneo mbalimbali nchini na kwa kuanzia
vinajengwa vituo 24 katika maeneo ya kimkakati ili kutengemaza gridi
ya Taifa.
Aidha, ameishukuru Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB) kwa kutoa mkopo wa
masharti nafuu wa kiasi cha Dola za Marekani milioni 140 ili
kutekeleza mradi wa Malagarasi ambapo Serikali ya Tanzania imetoa
Dola za Marekani Milioni 4.14. Amesema Benki hiyo imeendelea kuiunga
mkono Serikali katika miradi mbalimbali nchini.
Vilevile, amewaagiza Wakandarasi kutekeleza mradi huo kwa haraka na
ufanisi kama ilivyo kwa mradi wa umeme wa JNHPP ili wananchi wa Kigoma
na nchi nzima wapate umeme wa uhakika.
Mradi wa Malagarasi unahusisha ujenzi wa eneo la kufua umeme wa maji,
njia za kupitisha maji, jumba la mitambo ya umeme, kituo cha kupokea
na kusafirisha umeme, ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme ya msongo wa
kV 132 ambayo itaunganishwa kwenye Gridi ya Taifa kupitia kituo cha
Kidahwe- Kigoma na kuunganisha umeme kwenye vijiji 7 vitakavyopitiwa
na mradi.
Akizungumza kabla ya utiaji Saini, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri
Mkuu, Kazi, Ajira na WenyeUlemavu Mhe. Profesa Joyce Ndalichako
amesema mbali na uzalishaji wa megawati 49.5 kuongeza kiwango cha
umeme katika gridi ya Taifa, pia hatua hiyo itachochea anzishaji na
ukuaji wa viwanda katika mkoa wa Kigoma.
Ameongeza kuwa kupitia hali hiyo, ajira zitaongezeka na kuwezesha
wananchi kushiriki katika kukuza Uchumi wa Mkoa wa Kigoma na Taifa kwa
ujumla.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Thobias Andengenye amesema
maono na maelekezo ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kuhusu uzalishaji
wa nishati mkoani humo yameuheshimisha Mkoa wa Kigoma na Taifa kwa
ujumla.
Amesema uzalishaji wa megawati 49.5 za umeme utapunguza gharama za
uendeshaji ambapo kwa sasa zinatumika lita 28,000 za mafuta kwa siku
kwa ajili ya kuzalisha umeme.
Viongozi wengine walioshuhudia utiaji Saini ni Mkuu wa Mkoa wa Dodoma,
Rosemary Senyamule, Wabunge kutoka Mkoa wa Kigoma Katibu Mkuu wa
Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba na Makamu Mwenyekiti wa
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Mhe.Kilumbe Ng’enda.

.jpg)