Wakazi wa mkoa wa Katavi wametakiwa kutovamia na kuharibu mifumo ya chanzo cha maji mto Katuma kwakuwa kufanya hivyo inaathiri rasilimali za misitu na wanyama hususani viboko.
Akizungumza na Mwananchi leo Alhamis Februari Mosi 2024 Msimamizi wa bonde la maji mto Katuma Mathew Edson amesema changamoto hiyo inasababishwa na baadhi ya watu kuvamia na kuanzisha shughuli za kilimo,ufugaji na ukataji miti ovyo.
“Uharibifu ni mkubwa tunajitahidi kuhifadhi kwa kutumia Jumuiya zinazoshirikiana na uongozi wa vijiji angalau kwasasa tatizo limepungua,”
“Kidakio cha Katuma kina mito mitatu,mto mama Katuma,Mpanda na Msaginya,tulifanikiwa kuzibua vibanio haramu 46 vilivyosababisha upotevu wa maji mkubwa,”amesema Edson
Amesema maji hayo yanalikuwa yanayokwenda mashambani bila mpangilio wowote na kwamba ilisababisha viboko kukosa maji wakati wa kiangazi.
Mwakilishi Meneja mradi wa Sustain Eco unaofadhiliwa na Ubalozi wa Swiden ili kuboresha mifumo ya Ikolojia mkoani Katavi Fadhil Njilima amesema wamebaini kuna changamoto kubwa ya uvamizi wa mito.
“Kuna matatizo makubwa katika maeneo hayo hasa umwagiliaji usio endelevu, uvamizi wa misitu kwaajili ya ufugaji na kilimo usiofuata sheria,”
“Tunachokifanya ni kuielimisha jamii kuona umhimu wa kutunza rasilimali hizo ili mfumo wa ikolojia ufanye kazi vizuri na uzalishaji uwe endelevu,”amesema Njilima
Baadhi ya wakazi wa mkoa wa Katavi Diana Maico amesema uelewa wa jamii katika masuala ya uhifadhi upo kiwango cha chini kutona na ukosefu wa elimu.
“Wanakwenda kulima kwenye maeneo yaliyotengwa kuhifadhia kwa kigezo cha kufuata ardhi yenye rutuba inachangiwa pia na watu kukosa mbinu za kilimo cha kisasa,”
“Hawanunui pembejeo kwa makusudi ama kwa kukosa uwezo au wanataka kulima mashamba makubwa sana ambayo ndani ya kijiji hayapo wabadilike,”amesema Diana
