Jeshi la polisi mkoani Katavi limewahakikishia wanahabari wote kuwa litalinda usalama wao wakati wa utekelezaji majukumu yao huku likiwasisitiza kutoandika habari pasipo kuzishirikisha mamlaka husika.
Kauli hiyo imetolewa na Kamanda wa polisi mkoa wa Katavi Kaster Ngonyani wakati akifunga mdahalo baina ya polisi na wanahabari uliolenga kudumisha mahusiano ya utendaji kazi wao.
“Tutawalinda fanyeni kazi vizuri polisi tupo nyuma yenu lakini matukio yanayotokea yote hakikisheni mnanijulisha mimi Kamanda wa polisi Katavi,”
“Ili niwapatie taarifa nzuri msipofanya hivyo mtasababisha taharuki kubwa katika jamii kwasababu mtatoa taarifa za uongo katika Jamii,”amesema Ngonyani.
Awali Mwenyekiti wa chama cha wandishi wa habari mkoa wa Katavi Walter Nguruchuma ameishukru UTPC kuona umhimu wa kuwawezesha wanahabari kuwakutanisha na polisi kupitia mdahalo huo.
“Tumejenga mahusiano mazuri, tunalishukru pia polisi kwa ushirikiano waliotupatia tangu mdahalo wa kwanza hadi huu wa tatu,”amesema Nguruchuma.
“Kuna mambo mengi tulikuwa hatuyafahamu na polisi walikuwa hawayajui lakini kwasasa tumeyafahamu,kwasasa tutafanya kazi vizuri zaidi tofauti na hapo awali,”
Aidha amesema ushirikiano huo wa polisi na wanahabari uendelezwe katika utendaji kazi ili kujenga Imani kwa jamii, wasipoaminika utendaji kazi utakuwa mgumu.
“Yale tuliyoazimia kupitia mdahalo huu tuyaenzi yasiishie humu ndani,”amesema. Mrakibu Mwandamizi wa jeshi la polisi mkoa SSP.Juma Jumanne ameipongeza klabu ya wandishi wa habari mkoa wa Katavi kwakubuni na kuanzisha kwa maslahi ya jamii.
“Inaleta ujenzi mzuri wa jamii yetu, nia kubwa ambayo tunaona ni kupeana taarifa lakini nia ni kudumisha amani,usalama yale mnayoripoti yalete maendeleo ushirikiano huu uwe endelevu,”amesema Jumanne.
Sanjari na hayo baadhi ya wanahabari wa mkoa wa Katavi wameishukru UTPC kutoa fursa hiyo wakiahidi kuendelea kufanya kazi kwaushirikiano na polisi.
“Tutafanya kazi kwa weledi kama maadili yanavyoelekeza hususani wakati huu tukielekea katika uchaguzi wa serikali za mitaa na mengineyo,”wamesema baadhi yao.
Mwisho
