Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip
Mpango amezielekeza Wizara ya Afya, Ofisi ya Rais - TAMISEMI na Mamlaka
nyingine zinazohusika kuhakikisha kunakuwepo na usimamizi madhubuti wa
Mpango Jumuishi wa Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii ili uweze kufikia
malengo yaliyokusudiwa.
Makamu wa Rais amesema hayo wakati wa uzinduzi wa Mpango Jumuishi wa
Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii uliyofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha
Mikutano cha Julius Nyerere Jijini Dar es salaam. Amesema ni lazima kuweka
mfumo mzuri wa uratibu wa shughuli za mpango huo na kuhakikisha taarifa
za utekelezaji zinapatikana ikiwemo kutumia mifano ya kidijitali.
Makamu wa Rais amewasihi wahudumu wa afya watakaopewa dhamana ya
kutekeleza jukumu hilo kuzingatia weledi na kujituma pamoja na kutoa rai
kwa jamii kuupokea mpango huo na kuthamini huduma za wahudumu wa
afya ngazi ya jamii kwa kuwapa ushirikiano wa kutosha ili kulinda na
kuboresha afya katika jamii.
Halikadhalika Makamu wa Rais amesisitiza masuala ya lishe bora na usafi wa
mazingira yasiachwe nyuma katika kutekeleza Mpango huo kama njia
mojawapo ya kujenga afya na kudhibiti magonjwa ambayo yanatokana na
uchafuzi wa mazingira ikiwemo kipindupindu na malaria. Ametoa wito kwa
Jumuiya ya Kimataifa, Wadau wa Maendeleo na Wadau wengine kuunga
mkono juhudi za Serikali pamoja na vipaumbele vya Mpango huo
vilivyoainishwa wakati wote wa utekelezaji.
Vilevile Makamu wa Rais amewasihi viongozi wote wanaohusika katika ngazi
zote kuhakikisha zoezi la kuwachagua Wahudumu wa afya ngazi ya jamii
linafanyika kwa kufuata vigezo na taratibu zilizowekwa ili kupata Wahudumu
wenye sifa stahiki watakaotekeleza majukumu hayo. Amewataka
watakaopewa jukumu la kutekeleza mpango huo, kujiepusha na vitendo vya
upendeleo, rushwa au ukiukwaji wa taratibu.
Amesema Serikali ya Awamu ya Sita imepanga kuajiri na kuwajengea uwezo
jumla ya Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii wapatao 137,294 katika Mikoa
yote 26 ya Tanzania Bara ambapo Utekelezaji wa Mpango huo utafanyika
katika kipindi cha miaka mitano kwa awamu ambapo katika mwaka wa
kwanza (2023/24) zaidi ya Wahudumu 28,000 watafikiwa na baadaye wastani
wa Wahudumu 27,324 kila mwaka kwa kipindi cha miaka minne mfululizo
kuanzia mwaka 2024/25 hadi 2027/28. Jumla ya shilingi bilioni 899.4
zinatarajiwa kutumika katika kutekeleza mpango huo kwa kipindi cha miaka
mitano.
Kwa upande wake Waziri wa Afya Ummy Mwalimu amesema Mpango huo
umelenga kupunguza idadi ya wagonjwa katika vituo vya kutolea huduma za
afya kwa kuimarisha huduma za afya kinga pamoja na kuongeza tija na
ufanisi katika kutoa huduma za afya kufikia lengo la afya kwa wote.
Ameongeza kwamba Mpango huo utasaidia kukabiliana na upungufu wa vituo
vya kutolea za afya hususani katika maeneo ya vijijini. Aidha amesema kupitia
mpango huo wahudumu wa afya ngazi ya jamii wameweza kuibua magonjwa
mbalimbali yanayoikabili jamii kama vile Kifua Kikuu, Kipundupindu na
ugonjwa wa Marburg.
Amesema kupitia mpango huo wataweza kupunguza gharama za matibabu
kutokana na kutambulika kwa ugonjwa katika hatua za awali zaidi. Amesema
umuhimu wa wahudumu hao ngazi ya jamii ni daraja kati ya vituo vya kutolea
huduma na jamii husika kwa kuwa wamekuwa wakitambua mapema maradhi
yanayojitokeza.
Waziri Ummy amesema katika kuchagua wahudumu wa afya ngazi ya jamii
suala la wakazi wa eneo husika litazingatiwa ili kuendana na mila na desturi za
wananchi wa eneo hilo.
Imetolewa na
Ofisi ya Makamu wa Rais
31 Januari 2024
Dar es salaam.

