Katika jitihada za kuhakikisha maeneo yote nchini yanapata umeme wa uhakika,
Serikali imeshaanza kutekeleza mradi wa kupeleka umeme wa Gridi katika Mkoa
wa Rukwa kupitia mradi wa TAZA ulioanza kutekelezwa mwezi Novemba, 2023
na unatarajiwa kukamilika Mwezi Agosti, 2026.
Hayo yameelezwa leo bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Nishati, Mhe.
Judith Kapinga wakati akijibu swali la Mbunge wa Nkasi, Mhe. Aida Khenani
aliyetaka kufahamu mkakati wa kumaliza changamoto ya upatikanaji umeme
wilayani Nkasi Mkoa wa Rukwa.
Amesema kuwa, kwa sasa TANESCO inaendelea kufanya maboresho ya
miundombinu ili kupunguza changamoto ya upatikanaji umeme mkoani humo na
kujenga kituo kipya cha kupoza umeme.
Kuhusu hali ya upatikanaji umeme nchini amesema kuwa, upungufu wa umeme
unaendelea kupungua akitaja takwimu kuwa, upungufu umepungua kutoka
megawati 400 hadi 144 kwa siku ya leo.
Ameeleza kuwa, Serikali inaendelea kufanya juhudi mbalimbali ili kuboresha hali
ya upatikanaji umeme nchini akitolea mfano utekelezaji wa Mradi wa umeme wa
Julius Nyerere (JNHPP) ambao inatarajiwa kuwa, katika mwezi wa Pili kuelekea
Machi mwaka huu utaanza kuingiza megawati 235 katika Gridi ya Taifa.
Mhe. Kapinga pia amezungumzia kazi ya upelekaji umeme wa gridi mkoani
Katavi ambapo ameeleza kuwa, tayari kuna mradi unaoendelea kutekelezwa na
kwa sasa baadhi ya vituo vya kupoza umeme vimekamilika na hivyo, nguvu
sasa inawekwa zaidi katika ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme kwenda mkoani
humo.
Cap
Moja
Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga akijibu maswali mbalimbali ya
Wabunge, bungeni jijini Dodoma tarehe 1 Februari, 2024.
