Serikali imesema imeanza hatua za kujenga ukuta katika eneo la Nungwi
Zanzibar kwa ajili ya kusaidia kuzuia maji ya bahari kuingia kwenye makazi
kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis
Hamza Khamis amesema hayo wakati akijibu maswali bungeni jijini Dodoma
leo Februari 01, 2024.
Akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Nungwi Mhe. Simai Hassan Sadiki
aliyetaka kujua kama eneo hilo limekidhi vigezo vya kujengewa ukuta
kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Mhe. Khamisi alisema kuwa Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais
inatekeleza miradi ya ujenzi wa kuta katika fukwe mbalimbali za bahari
Tanzania Bara na Zanzibar.
“Eneo ambalo linapaswa kujengwa ukuta limekidhi vigezo na lina kila sababua
ya kufanyiwa hivyo, tumeanza kufanya utafiti na ndio maana viongozi wa SMT
na SMZ wamekwishafika pale na tumeombea bajeti hivyo Serikali ina kila
sababu ya kulifanyia kazi eneo hilo,“ alisema.
Akijibu swali la msingi la mbunge huyo, Naibu Waziri Khamis alisema kuwa
Serikali itaendelea kubaini maeneo yenye changamoto kubwa ya uharibifu wa
mazingira na kuyaweka katika kipaumbele ili kuyatafutia rasilimali fedha kwa
ajili ya kuitatua.
Akiendelea kujibu swali hilo amesema kuwa mabadiliko ya tabianchi yanazidi
kusababisha athari katika maeneo mbalimbali nchini yakiwemo ya ukanda wa
pwani nchini.
Katika kubainisha maeneo yaliyoathirika na kuyaweka katika vipaumbele,
alisema Serikali inafanya tathmini ya kiwango cha uharibifu na athari
zitakazojitokeza hii ni moja ya sababu ya mojawapo ya vigezo vinavyotumika
kuweka vipaumbele maeneo yaliyoathirika katika mipango ya utekelezaji
Kwa upande mwingine alitoa rai kwa wananchi kuacha kufanya shughuli
zinazoharibu mazingira ya visiwa zikiwemo uvuvi usio endelevu na kilimo cha
mwani kinachoharibu mazingira