Na Gideon Gregory, Dodoma.
Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Dkt. Samwel Gwamaka amesema kuwa baraza hilo limetoa Jumla ya Vibali 174 vya kushughulika na taka hatarishi ndani ya Nchi ambapo vibali 10 vya kuingiza na kusafirisha nje ya Nchi na kupelekea kiasi cha Tani 516,041 za taka mbalimbali kukusanywa na makampuni yenye vibali.
Dkt. Gwamaka ameyasema hayo leo Machi 3,2023Jijini Dodoma wakati akieleza mafanikio ya Baraza hilo mbele ya waandishi wa habari katika kipindi cha miaka miwili ya Utawala wa serikali ya awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Amesema katika kipindi cha Julai 2021 hadi Februari 2022 baraza hilo lilimepokea na kushughulikia malalamiko takribani 369 ya Uchafuzi na Uharibifu wa Mazingira kutoka kwa wananchi ikiwemo kuvuja kwa mafuta kutoka kwenye mabomba ya mafuta, kuchoma taka hatarishi chini ya kiwango kinachotakiwa kisheria.
“Malalamiko haya yalihusisha uchafuzi wa vyanzo vya maji, utiririshaji wa maji taka ,uchafuzi wa hewa kutokana na shughuli za viwandani, kelele za muziki, kushamiri kwa gereji bubu maeneo ya makazi, kushamiri vituo vya mafuta katikati ya makazi ya watu, matumizi ya mifuko ya plastiki iliyokatazwa na kutapakaa maeneo ya makazi na tumehakikisha tunatoa elimu elimu sahihi na suluhisho juu ya jambo hili kwa wananchi,”amesema.
Sanjari na hayo pia Dkt. Gwamaka ameongeza kuwa NEMC imefanikiwa kusajili miradi 1702 ambapo kati yake 967 ni ya (TAM) na 735 ni ya ukaguzi wa Mazingira.
"Kwa kupitia taarifa ya Tathimini ya Athari kwa Mazingira katika kipindi cha Julai 2021 hadi Februari 2022 Baraza limefanikiwa kusajili miradi 1702 ambapo kati yake 967 ni ya {TAM} na 735 ni ya ukaguzi wa Mazingira" ameongeza.
Amesema kukusanywa huko kwa tani 516,041 za taka kunaonesha jinsi baraza hilo linavyowajibika katika kuhakikisha sheria ya Mazingira inayozingatia uhifadhi na utunzaji wake unazingatiwa na wametoa jumla ya vibali 174 vya kushughulika na taka hatarishi ndani ya nchi.
