MAKUMBUSHO YA KIMONDO CHA MBOZI KUZINDULIWA KESHO.

MUUNGANO   MEDIA
0

 


 Uongozi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA)  kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Songwe  kesho Jumamosi  Machi 4, 2023 unatarajia kufungua  Makumbusho ya Kimondo yaliyopo katika Kijiji cha Ndolezi katika  Wilaya ya Mbozi  mkoani Songwe.

Kimondo cha Mbozi  ni moja ya kivutio bora cha utalii katika Mkoa wa Songwe na ni  miongoni wa vimondo vizito kumi vinavyojulikana duniani na cha pili kwa ukubwa barani Afrika.

Akitoa taarifa ya ufunguzi  huo leo Machi 3 Afisa Uhifadhi Mkuu wa Uhusiano wa NCAA, Joyce Mgaya amesema ufunguzi wa Makumbusho hayo ni  miongoni mwa hatua za kuunga mkono jitihada za Serikali katika kukuza Utalii katika mikoa ya Nyanda ya juu Kusini na pia kuimarisha uhifadhi wa urithi tulionao wa mila na tamaduni zetu.

''Ufunguzi wa Makumbusho hii ni fursa ya kujivunia na kuenzi tamaduni hususan wananchi wa Mkoa wa Songwe. Nawaomba wakazi wa Mkoa wa Songwe mjitokeze kwa wingi kushuhudia ufunguzi huo "amesema Mgaya .

Amefafanua kuwa kukamilika kwa Makumbusho  licha ya kuhifadhi taarifa za kimondo hicho pia Makumbusho hiyo itasaidia kuhifadhi mila na tamaduni za makabila ya watu wa Nyanda za Juu  Kusini hususan kabila Wanyiha, Ndali na Wanyamwanga. 

Afisa huyo wa Uhusiano ameongeza kuwa siku ya kesho wageni mbalimbali wa ngazi ya Taifa, mkoa, na wilaya wanatarajia kushiriki katika ufunguzi huo ikiwemo Bodi ya Wakurugenzi wa NCAA wakiongozwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Jenerali Venance Mabeyo ( Mstaafu). 

Aidha, Mgaya  amesema  mara baada ya ufunguzi wa Makumbusho hayo kutafuatia na tukio la kutembelea program maalum ya elimu ya anga pamoja na kutembelea kivutio kingine cha  utalii cha maji moto kilichopo  katika eneo la Nanyala.

Kimondo cha Mbozi kiligunduliwa na Muafrika aliyejulikana kwa jina la Mzee Halele ambaye alikuwa Mhunzi hivyo katika harakati zake za kutafuta chuma alikiona kimondo hicho na baadae kumbukumbu za kimondo hicho ziliwekwa kwenye maandishi na Mzungu aliyeitwa Wiliam Nolt mwaka 1930.

Tags

Chapisha Maoni

0Maoni
Chapisha Maoni (0)