Changamoto ya wakazi wa Wilaya ya Bukombe mkoani Geita ya kufuata maji umbali mrefu hatimae inaelekea mwisho baada ya Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Wilaya ya Bukombe Mkoani Geita kupeleka miradi ya maji katika maeneo yao.
Wanachi hao wameeleza kuhusu changamoto ya kupata maji safi na salama kutokana na kukosa huduma ya maji kwa muda mrefu.
Wameipongeza Serikali kwa miradi ya maji inayotekelezwa na RUWASA wilaya ya Bukombe kwasababu miradi hiyo itakapo kamilika itasaidia kwa kiasi kikubwa kuondoa changamoto hiyo.
Meneja wa RUWASA Wilaya ya Bukombe Mhandisi James Moise amesema hali ya upatikanaji wa maji imefikia asilimia 46.2 huku wakiendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya maji katika wilaya hiyo.
Amesema kwa sasa RUWASA wilaya ya Bukombe inatekeleza miradi zaidi ya tisa ikiwa imefikia zaidi ya asilimia 70 huku mingine ikiwa hatua za mwisho ili kuanza kutoa huduma ya maji kwa wananchi.
Mhandisi James amesema miradi hiyo itakapokamilia itasaidia kwa kiasi kikubwa kuongeza wigo wa upatikanaji wa maji vijijini kutoka asilimia 46.2 hadi kufikia asilimia 65.
Meneja wa RUWASA mkoa wa Geita mhandisi Jabiri Kayilla amesema kwa mwaka wa fedha 2022/23 mpaka sasa serikali imetoa kiasi cha bilioni moja kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maji wilayani Bukombe.
Mhandisi Kayilla amesema pamoja na kusimamia miradi ya maji katika Mkoa wa Geita wanaendelea kuimarisha vyombo vya watoa huduma ya maji ngazi ya jamii (CBWSO’s) ili kuhakikisha miradi ya maji inayotekelezwa mkoani humo itakapokamilika iweze kutumika vyema kwa wananchi.

