Na Gideon Gregory, Dodoma.
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usalama na Afya mahali pa Kazi (OSHA), Khadija Mwenda, amesema kuwa Wakala huo umefanikiwa kuongeza idadi ya maeneo ya kazi yaliyosajiliwa kutoka 4,336 hadi 11,953 ikiwa ni sawa na asimilia 276.
Bi. Mwenda ameyasema hayo leo Machi 4,2023 Jijini Dodoma katika mkutano na waandishi wa habari, ambapo amesema idadi ya kaguzi zilizofanyika zimeongezeka kutoka kaguzi 104,203 hadi kufikia kaguzi 322,241 sawa na asilimia 132.
“Halikadhalika, kumekuwa na ongezeko la asilimia 175 ya wafanyakazi waliopata mafunzo ya usalama na afya mahali pa kazi kutoka wafanyakazi 32,670 hadi kufikia wafanyakazi 43,318, mafunzo haya yanajumuisha mafunzo ya usimamizi wa masuala ya usalama na afya mahali pa kazi na uundwaji wa kamati za Usalama na Afya (Health and Safety Managemnet System), mafunzo ya kufanya kazi za mazingira ya juu (working at height), mafunzo ya huduma ya kwanza, mafunzo ya usimamizi na udhibiti wa kemikali katika maeneo ya kazi, mafunzo ya usalama na afya katika sekta ya mafuta na gesi na katika sekta ya ujenzi na majenzi na mafunzo ya usalama wa mitambo,”amesema.
Aidha, ameongeza kuwa kumekuwa na ongezeko la upimaji afya za wafanyakazi kwa asilimia 320 kutoka 363,820 hadi kufikia 1,112,237 waliopimwa katika kipindi tajwa.
“Ongozeko hilo lilitokana na kupunguza ada mbalimbali na kuboresha mifumo ya usimamizi ambayo imewezesha maeneo mengi ya kazi kukaguliwa, wafanyakazi wengi kupimwa afya na mafunzo mbalimbali kufanyika, ongezeko hili ni tafsiri kwamba hali ya usalama na afya katika maeneo ya kazi inazidi kuimarika,”ameongeza.
Amesema katika kusimamia Sheria ya Usalama na Afya kwa lengo la kuzuia ajali, magonjwa na vifo vitokanavyo na kazi, maeneo ya kazi ambayo hayakuzingatia Sheria na Kanuni za Usalama na Afya yalichukuliwa hatua mbali mbali za kisheria zikiwemo kupewa hati ya maboresho (Improvement Notice) ambapo maeneo ya kazi 1,588 yalipewa hati hizo na maeneo ya kazi mengine 105 yalitozwa faini.
Akizungumzia mipango ya OSHA, Bi Mwenda amesema Wakala umejipanga kuendelea kutenga fedha kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vya kisasa vya ukaguzi vinavyoendana na mabadiliko ya teknolojia pamoja na kujenga miundombinu muhimu ya kutolea huduma za Usalama na Afya zikiwemo maabara za kisasa za uchunguzi wa sampuli mbali mbali zinazochukuliwa katika sehemu za kazi, na miundombinu ya kutolea mafunzo.
“Wakala unakusudia kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusiana na umuhimu wa kufanya shughuli mbali mbali kwa kuzingatia kanuni bora za Usalama na Afya pamoja na kuendesha majadiliano na wadau juu ya utekelezaji wa Sheria ya Afya na Usalama Mahali pa Kazi kupitia semina, mikutano, makongamano na maonesho mbalimbali,”amesema.
