KAMPUNI ya Mbolea Tanzania (TFC) imesema kiwanda chake kipya cha kisasa kinachotarajiwa kujengwa mkoani Tanga kitakuwa na uwezo wa kuzalisha mbolea zinazokidhi mahitaji halisi ya udongo wa maeneo mbalimbali nchini, hatua inayolenga kuongeza tija kwa wakulima na kuimarisha uzalishaji wa mazao.
Akizungumza katika kilele cha maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma jijini Dodoma, Mkurugenzi wa Huduma za Taasisi wa TFC, Nuru Mhando, amesema kiwanda hicho kitatumia teknolojia ya upimaji wa udongo ili kubaini kiwango cha rutuba kabla ya kuzalisha mbolea inayofaa kwa eneo husika.
Amesema matumizi ya mbolea zinazozingatia mahitaji ya udongo yatasaidia wakulima kupata matokeo bora zaidi katika uzalishaji, kuongeza mavuno na kutumia pembejeo kwa ufanisi mkubwa.
Kwa mujibu wa Mhando, mradi huo pia utachangia kupunguza utegemezi wa mbolea kutoka nje ya nchi na kupunguza gharama za uagizaji, huku ukihakikisha upatikanaji wa mbolea bora kwa wakati unaohitajika.
Ameeleza kuwa TFC inaendelea kusambaza mbolea kwa wakulima kupitia mfumo wa ruzuku wa serikali unaolenga kuwasaidia kupata pembejeo hizo kwa bei nafuu. Hadi sasa, kampuni hiyo imesambaza zaidi ya tani 49,000 za mbolea za kupandia na kukuzia mazao kwa wakulima nchini.
Mbali na usambazaji wa mbolea za mazao ya chakula na nafaka, TFC pia imekuwa ikitoa mbolea kwa wakulima wa tumbaku, moja ya mazao ya kimkakati yanayochangia uchumi wa taifa.
Aidha, kampuni hiyo inaendelea kutoa mafunzo kwa wakulima kuhusu matumizi sahihi ya mbolea ili kuongeza tija na kuhakikisha pembejeo hizo zinatumika kwa manufaa makubwa zaidi.
Mhando amesema TFC itaendelea kutoa elimu na kushughulikia changamoto zinazowakabili wakulima ili kuongeza uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara, hatua itakayosaidia kuimarisha usalama wa chakula na kukuza uchumi wa wananchi.
