Na Avelina Musa - Dodoma.
KATIKA juhudi za kuwakomboa wanawake wa Vijijini kiuchumi na kijamii Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) umesema unaendelea kuwaelimisha na kuwawezesha wanawake kupitia miradi inayohamasisha usawa wa kijinsia, uongozi wa wanawake na kilimo ikolojia.
Hayo yamesemwa leo 05.8.2026 na mwakilishi kutoka Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) Bi. Mwajuma Mkombozi wakati wa mahojiano na waandishi wa habari katika Viwanja vya Maonesho ya 88 jijini Dodoma, amesema taasisi hiyo imejikita katika nguzo tatu kuu ambazo ni wanawake na uongozi, usawa wa kijinsia na kilimo ikolojia.
Amesema TGNP kupitia miradi yake imefanikiwa kuwezesha wanawake wa vijijini kutumia mbegu za asili zinazotokana na wakulima wenyewe, pamoja na mbinu za kilimo ikolojia zinazoongeza uzalishaji huku zikihifadhi mazingira na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Aidha,Bi Mwajuma amewataka wananchi kutembelea banda la TGNP ili kujifunza kuhusu afua mbalimbali zinazotekelezwa na taasisi hiyo, ikiwemo elimu ya kilimo ikolojia, usawa wa kijinsia na uongozi.
Hata hivyo kwa Upande wake Mratibu wa vituo vya Taarifa na Maarifa Mkoa wa Kilimanjaro Bi. Stella John ambaye pia ni mkulima kiongozi ameeleza namna afua ya kilimo ikolojia ilivyoleta tija katika kupata mbegu za wanawake wa vijijini na kuleta mabadiliko.
"Kila mwanamke ndiye kiongozi moja kwa moja kwenye utunzaji wa mbegu na kuhakikisha usalama wa chakula kwa sababu kuanzia mwanzo wanawake walikuwa wakisimamia mfumo wa uhakika wa chakula kwenye kaya, lakini pia kutunza mbegu na kutafuta mbegu ambazo hazipo kwenye familia au jamii yake." Amesema Bi stela John
Amesema kuwa kutokana na mabadiliko ya tabia ya nchi, wanawake wengi wamejifunza namna ya kuikinga familia na shida ya chakula kwa kutambua aina ya mbegu za kupanda kutokana na mabadiliko ya tabia ya nchi.
Bi.Stella ametoa wito kwa wanawake kujipambania kwa kuwa wao ni msingi wa familia na wana uwezo wa kuhakikisha usalama wa chakula kwenye familia na akibainisha kuwa ili familia iwe na amani ni lazima kuwe na uhakika wa chakula.
Bi stella pia ameshiriki mjadala uliohusisha wadau mbalimbali wa kilimo uliofanyika kwenye ukumbi wa wizara ya kilimo ambapo alichangia mada juu ya umuhimu wa mwanamke kwenye utunzaji wa mbegu.







