WIZARA YA AFYA YAAZIMIA KUIMARISHA USALAMA WA AFYA NCHINI KUPITIA UTEKELEZAJI IMARA WA KANUNI ZA AFYA ZA KIMATAIFA (IHR 2005)

MUUNGANO   MEDIA
0



Na Mwandishi wetu,ARUSHA

Wizara ya Afya Tanzania imeendelea kuimarisha utekelezaji wa Kanuni za Afya za Kimataifa (IHR 2005) zilizoboreshwa mwaka 2024, kupitia kikao kazi cha robo mwaka kinacholenga kutathmini maendeleo na kuimarisha uwezo wa nchi katika kukabiliana na matishio ya afya ya umma.




Kikao hicho cha siku nne kinachofanyika mkoani Arusha kimewakutanisha wataalamu kutoka sekta mbalimbali, kwa lengo la kujadili hatua zilizofikiwa, changamoto zilizopo na kuweka mikakati ya pamoja ya kuimarisha usalama wa afya nchini.

Akifungua kikao hicho, Mkurugenzi Msaidizi wa Sehemu ya Epidemiolojia na Udhibiti wa Magonjwa kutoka Wizara ya Afya Tanzania, Dkt. Vida Makundi Mmbaga, amesema utekelezaji thabiti wa Kanuni za Afya za Kimataifa ni msingi muhimu wa kuimarisha utayari wa nchi katika kuzuia, kugundua na kukabiliana na milipuko ya magonjwa pamoja na dharura nyingine za afya ya umma.



"Serikali imeendelea kuimarisha mifumo ya ufuatiliaji wa magonjwa, mawasiliano ya hatari, huduma za maabara, udhibiti wa maambukizi na maandalizi ya dharura, ili kuhakikisha nchi inakuwa na uwezo wa kujibu kwa haraka matukio yoyote yanayoweza kuhatarisha afya ya wananchi", amesema Dkt. Mbaga

Kikao hicho kinaratibiwa na Wizara ya Afya Tanzania kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu Tanzania pamoja na Shirika la Afya Duniani (WHO) Tanzania kupitia mradi wa Pandemic Fund, ambao unalenga kuimarisha uwezo wa nchi katika kuzuia na kukabiliana na majanga ya milipuko.



Dkt. Mmbaga amesisitiza pia umuhimu wa ushirikiano wa sekta mbalimbali na ushiriki wa wananchi katika mfumo wa ufuatiliaji wa magonjwa, akieleza kuwa jamii ina nafasi kubwa katika kutoa taarifa mapema kuhusu matukio yoyote yasiyo ya kawaida ya kiafya.


Amefafanua kuwa wananchi wanapaswa kutoa taarifa za tetesi za magonjwa kwa kupiga simu bure namba 199, hatua inayosaidia mamlaka za afya kufanya uchunguzi wa haraka, kudhibiti maambukizi na kuzuia kuenea kwa magonjwa ya mlipuko.

Aidha, amesisitiza kuwa ushiriki wa wananchi katika kutoa taarifa kwa wakati ni nguzo muhimu ya mfumo wa ufuatiliaji wa magonjwa nchini, huku akibainisha kuwa hadi sasa Tanzania haijaripotiwa kuwa na kisa chochote cha ugonjwa wa Ebola.

Kikao hicho cha siku nne, kinachofanyika kuanzia Juni 22 hadi 25, 2026, kinaendelea kujadili njia bora za kuimarisha mifumo ya taifa katika kuzuia na kudhibiti magonjwa ya mlipuko pamoja na dharura nyingine za kiafya, kwa lengo la kulinda afya ya wananchi na kuimarisha usalama wa afya ya umma kwa ujumla.





Chapisha Maoni

0Maoni
Chapisha Maoni (0)