HUDUMA ZA KINGA NI MHIMILI WA USALAMA WA AFYA NCHINI – DKT. GOWELLE

MUUNGANO   MEDIA
0




Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Huduma za Kinga kutoka Wizara ya Afya, Dkt. Otilia Gowelle, amesema huduma za kinga zina nafasi ya msingi katika kuimarisha usalama wa afya nchini kwa kuzuia, kugundua mapema na kudhibiti matishio ya magonjwa hususan ya mlipuko kabla hayajaleta athari kubwa kwa jamii.


Akizungumza katika kikao kazi cha robo mwaka cha utekelezaji wa Kanuni za Afya za Kimataifa (IHR 2005), kinachofanyika mkoani Arusha kwa Uratibu wa Wizara ya Afya pamoja na Shirika la Afya Duniani ( WHO) kupitia Mradi wa Pandemic Fund Dkt. Gowelle amesema kuwa uwekezaji katika huduma za kinga ni hatua muhimu ya kujenga mfumo imara wa usalama wa afya unaoweza kukabiliana na milipuko ya magonjwa na dharura nyingine za afya ya umma.

Amesema Serikali kupitia Wizara ya Afya imeendelea kuimarisha huduma za kinga kwa kuboresha mifumo ya ufuatiliaji wa magonjwa, huduma za chanjo, na maandalizi ya kukabiliana na dharura za afya ili kuhakikisha wananchi wanalindwa dhidi ya matishio mbalimbali ya kiafya.

“Usalama wa afya huanza na kinga. Kadri tunavyoimarisha huduma za kinga, ndivyo tunavyojenga uwezo mkubwa zaidi wa kuzuia na kudhibiti magonjwa kabla hayajasababisha madhara makubwa kwa wananchi na taifa kwa ujumla,” amesema Dkt. Gowelle.

Halikadhalika, Dkt. Gowelle amepongeza Washiriki wa Kikao hicho huku ikiwemo Shirika la Afya Duniani(WHO) Tanzania kwani ni nguzo muhimu katika kuimarisha usalama wa afya hapa nchini.



Kikao hicho cha siku nne kinachofanyika kuanzia Juni 22 hadi 25, 2026, kimewakutanisha wataalamu kutoka Wizara ya Afya Zanzibar, sekta mbalimbali pamoja na wadau wa maendeleo ili kujadili mikakati ya kuendelea kuimarisha usalama wa afya nchini kupitia utekelezaji wa Kanuni za Afya za Kimataifa na huduma za kinga.




Wizara za Kisekta zinazoshirikiana ni pamoja, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira. Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu, Sehemu ya Maafa na majanga,Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI, Wizara ya Mifugo na Uvuvi pamoja na Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR), Vyuo Chuo Kuu MUHAS na SUA pamoja na mashirika ya WHO,FAO,UNICEF ,CIHEB, PATH na AMREF.






Chapisha Maoni

0Maoni
Chapisha Maoni (0)