ZAIDI YA BILION 113 YAIMARISHA HUDUMA YA MAJI SAFI SHINYANGA.

MUUNGANO   MEDIA
0

 



Na Avelina Musa - Dodoma.

Imeelezwa kuwa katika kipindi cha Uongozi wa Serikali ya awamu ya sita Mkoa wa Shinyanga umepokea kiasi cha shilingi bilioni 113.33 kwa ajili ya huduma ya maji safi ambapo huduma hiyo imeimarika kutoka asilimia 68 mwaka 2020 hadi asilimia 79 mwaka  2025.



Na fedha hizo zimeweza kuongeza idadi ya vijiji 222 vyenye huduma ya maji kutoka Vijiji 162 mwaka 2020 hadi Vijiji 384 mwaka 2025 na kukamilika kwa miradi 64 ambayo tayari kwa  kuanza kutoa huduma ya maji katika maeneo ya vijijini.



 Hayo yameelezwa  leo Julay 14,2025 Jijini Dodoma na Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga,Mhe.Mboni Mohamed Mhita wakati  akizungumza na waandishi wa habari akieleza mafanikio ya serikali ya awamu ya sita Chini ya Uongozi mahiri wa Rais Dkt Samia Suluhu Hassani.

Mhe.Mhita amesema Serikali inaendelea na utekelezaji wa mradi wa maji wa Ziwa Victoria katika Vijiji 111 katika maeneo ya Kishapu, Shinyanga na Kahama.

Akizungumzia sekta ya Afya amesema Mkoa wa Shinyanga umepokea kiasi cha  shilingi bilioni 79.1 kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya vituo vya kutolea huduma za Afya katika kipindi cha miaka minne ya serikali ya awamu ya sita.


Mhe.Mhita amesema Mafanikio yaliyopatikana ni pamoja na kuimarika kwa miundombinu ya kutolea huduma za afya, kuongezeka kwa upatikanaji wa dawa, vifaa,vifaa tiba na vitendanishi na kuimarika kwa upatikanaji wa huduma za afya karibu na wananchi.

"Mafanikio mengine ni Kukamilishwa kwa Hospitali ya Rufaa ya Mwawaza , Kuongezeka kwa idadi ya Hospitali za Wilaya 5 kutoka mbili mwaka 2020 hadi Saba mwaka 2025 katika Halmashauri za Shinyanga DC, Msalala DC, Ushetu DC, Shinyanga MC na Kishapu DC (Hospitali ya Mwadui), Kuongezeka kwa vituo vya afya 13 kutoka 25 mwaka 2020 hadi 38 mwaka 2025 vya Kambarage na Ihapa (Shinyanga MC).

"Kuongezeka kwa idadi ya zahanati 51 kutoka 226 mwaka 2020 hadi 277 mwaka 2025,Kuongezeka kwa nyumba 5 za watumishi wa afya kutoka 198 mwaka 2020 hadi 203 mwaka 2025 katika vituo vya Nyalwelwe,Chambo, Butibu (Ushetu DC), Msalala DH (Msalala DC) na Kuongezeka kwa upatikanaji wa dawa, vifaa, vifaa tiba na vitendanishi katika vituo vya kutolea huduma za afya kutoka asilimia 76 mwaka 2020 hadi asilimia 88 mwaka 2025,"ameeleza.

Kwa Upande wa Sekta ya Elimu amesema mkoa huo umepokea kiasi cha  shilingi bilioni 155.24 kwa ajili ya kujenga na kukarabati miundombinu ya elimu na kuongeza idadi ya walimu kwa shule za msingi, sekondari na vyuo vya kati ambapo imesaidia kuongezeka kwa uandikishaji na udahili wa wanafunzi, ufaulu pamoja na kupunguza umbali wa wanafunzi kufuata huduma ya elimu

"Mafanikio mengine ni pamoja na Kuongezeka kwa idadi ya shule za msingi 29 kutoka 682 mwaka 2020 hadi 711 mwaka 2025,Kuongezeka kwa idadi ya shule za sekondari 14 kutoka 186 mwaka 2020 hadi 200 mwaka 2025 na Kuongezeka kwa idadi ya vyumba vya madarasa 946 ya shule za msingi kutoka madarasa 4,940 mwaka 2020 hadi 5,886 mwaka 2025,"amesema.


Kwa upande wa umeme, Mkuu huyo wa Mkoa wa Shinyanga amesema vijiji vyote 506 vya mkoa huo sasa vimeunganishwa na umeme, huku miradi 133 ya usambazaji ikiendelea. Shirika la TANESCO limetumia bilioni 492 kufanikisha kazi hiyo, ikiwa ni pamoja na kugawa mitungi 6,500 ya gesi kwa ajili ya nishati safi ya kupikia.

Aidha amesema Katika kipindi cha miaka minne ya serikali ya awamu ya sita, Mkoa wa Shinyanga umepokea Shilingi trilioni 1.563 kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli za maendeleo katika sekta za afya, elimu, miundombinu ya usafiri na usafirishaji, maji, nishati, madini, kilimo, mifugo, viwanda, biashara, uwezeshaji wa wananchi kiuchumi na miradi ya kimkakati.







 
 

Chapisha Maoni

0Maoni
Chapisha Maoni (0)