Na Avelina Musa - Dodoma.
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050 Julai 17, 2025 Jijini Dodoma baada ya kukamilika kwa mchakato wa maandalizi uliodumu kwa takribani miaka miwili.
Hayo yameelezwa leo Julai 15,2025 na Katibu Mtendaji wa Tume ya Taifa ya Mipango,Dkt. Fred Msemwa wakati akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dodoma ambapo amesema maandalizi ya Dira hiyo yamefanyika kwa ushirikishwaji mpana wa wananchi na zaidi ya watanzania milioni 1.17 walitoa maoni yao kupitia njia mbalimbali huku zaidi ya watu 20,000 wakishiriki makongamano ya kitaifa.
Dkt. Fred Msemwa, amesema Dira hiyo inatarajiwa kuzinduliwa rasmi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika hafla itakayofanyika Julai 17, 2025, jijini Dodoma ambapo amesema maandalizi ya Dira hiyo yamechukua karibu miaka miwili, yakihusisha ushirikishwaji mpana wa wananchi kutoka makundi mbalimbali.
“Tulipokea maoni kutoka kwa Watanzania takribani milioni 1.174 kupitia njia mbalimbali, na zaidi ya watu 20,000 walihudhuria makongamano ya kitaifa yaliyolenga kuibua maono ya pamoja kuhusu mustakabali wa Taifa letu,” alisema Dkt. Msemwa
“Kazi ya ukusanyaji maoni ilifanyika kwa njia ya mbalimbali ikiwemo kupita kwenye familia moja moja,njia ya ujumbe wa simu njia ya makongamano na mikutano kwa takribani Kanda zote za Tanzania Bara na Zanzibar pamoja na njia ya mitandao ya kijamii,”amesema.
Dkt.Msemwa amesema Tume ilijifunza kutoka kwa nchi zilizofanikiwa kufikia uchumi wa kati, ili kubaini mbinu bora zinazoweza kutumika nchini, kabla ya kurejesha rasimu kwa wananchi kwa ajili ya uhakiki wa mwisho.
Amesema Dira hiyo ilijengwa kwa kuzingatia uzoefu na maarifa kutoka kwa nchi zilizoendelea kiuchumi kama Botswana ,Afrika Kusini,Brazil,Malaysia na Singapore kwa kupitia tafiti na mawasiliano ya moja kwa moja.
Aidha Dkt.Msemwa amesema Utekelezaji wa Dira hiyo utaanza rasmi Julai 2026 baada ya kumalizika kwa Dira ya Maendeleo ya 2025, ikiwa ni mwongozo mpya wa maendeleo kwa miaka 25 ijayo.



