Na Avelina Musa - Dodoma.
Mkuu wa Mkoa wa Tanga Balozi Dkt.Batilda Burian amesema kwa mujibu wa Takwimu za NBS kwa mwaka 2024, pato la Mkoa (GDP) limeongezeka kutoka wastani wa shilingi Trilioni 6.818 kwa mwaka 2020 hadi shilingi Trilioni 9.581 kwa mwaka, 2024 sawa na asilimia 4.7 ya Pato la Taifa ambalo ni shilingi Trilioni 205.846.
Amesema wastani wa pato la Mtu mmoja (Per Capital Income) limeongezeka kutoka wastani wa shilingi milioni 2.783,908.00 kwa mwaka 2020 hadi shilingi milioni 3,433,368.00 kwa mwaka, 2024 Ikiwa ni juu ya wastani wa kitaifa wa shilingi 3,204,244.00.
Balozi Batilda amesema hayo Leo Julay 15.2025 Jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari akitoa taarifa ya mafanikio ya serikali ya awamu ya sita katika mkoa wa Tanga ambapo amesema Takwimu hizo zinauweka Mkoa wa Tanga kushika nafasi ya sita (6) kati ya Mikoa yote ya Tanzania Bara katika vita dhidi ya umaskini pamoja na mchango wa pato la Taifa.
Amesema shughuli za kiuchumi na uzalishaji zinazotekelezwa na Wananchi wa Mkoa wa Tanga zipo kwenye maeneo mbalimbali zikiwemo Sekta za Kilimo, Mifugo, Uvuvi, Maliasili na shughuli nyingine za uzalishaji zinatokana na ukuaji wa Sekta ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji unaozingatia ujasiriamali katika sekta za umma na binafsi.
"Wananchi walio wengi zaidi ya asilimia 80 wamejikita katika shughuli za Kilimo, mifugo na uvuvi, asilimia tisa (9) wanajishughulisha na shughuli za mazao ya misitu, ufugaji nyuki na uchimbaji madini huku asilimia sita (6) wanajishughulisha na shughuli za biashara, uendeshaji wa viwanda,usafirishaji na uchukuzi na Sekta ya Fedha"Amesema Balozi Batilda.
Balozi Batilda amesema kwa kipindi cha Serikali ya awamu ya sita Mkoa wa Tanga umepokea fedha shilingi 3,091,742,180,252.12 (Trilioni 3.091) kwa ajili ya utekelezaji wa Miradi mbalimbali ya Maendeleo ya Kisekta.
Amesema Mafanikio yaliyopatikana katika uboreshaji wa huduma za Afya ikiwemo Ongezeko la Vituo vya kutolea Huduma za Afya, dawa na vifaa tiba limesaidia kuwasogezea wananchi huduma bora za Afya karibu na maeneo yao, hivyo kupunguza Vifo vya wakina mama na watoto kabla, baada na wakati wa kujifungua na umepunguza rufaa zisizo za lazima kwenda nje ya Mkoa.
"Mkoa wa Tanga katika kipindi cha mwaka 2020 hadi 2025 umeongeza vituo vya kutolea huduma za Afya vya serikali kutoka 325 hadi 417 ikiwa ni ongezeko la vituo 92,Zahanati zimeongezeka kutoka 287 hadi 361 sawa na ongezeko la zahanati 74,Amesema Balozi Batilda.
Balozi Batilda amesema kupitia fedha za ujenzi wa miundombinu ya Elimu zilizotolewa na Serikali, mafanikio mengi yamepatikana katika sekta ya Elimu ikiwemo ongezeko la ufaulu, idadi ya Shule pamoja na miundombinu ya shule ikiwemo,Ujenzi wa shule mpya, vyumba vya madarasa,nyumba za walimu, mabweni, mabwalo ambavyo vimerahisisha shughuli za ufundishaji wa wanafunzi katika shule za Msingi na Sekondari.
Aidha Balozi Batilda amesema Mradi wa kuboresha Miji (TACTIC) ambao utekelezaji wake upo katika Jiji la Tanga ambapo zitajengwa km 4 kwa kiwango cha lami, soko la samaki,soko la makorora, ukarabati wa fukwe raskazone na ujenzi wa mifereji yenye urefu wa km 4.

