Na Avelina Musa - Dodoma.
KATIKA Kuadhimisha siku ya mtoto wa Afrika, Shirika la Save the Children Nchini Tanzania limeishauri Serikali kuwapa kipaumbele watoto kwa kuwashirikisha katika kupanga bajeti kuanzia hatua ya chini Hadi Taifa.
Amesema ni vema Serikali iendelea kuboresha miundombinu ya sekta Afya na Elimu ili watoto waweze kusoma katika mazingira Bora na kutimiza malengo Yao.
Hayo yamesemwa na Afisa Mawasiliano wa Mradi kutoka Shirika la Save the Children Nchini Tanzania Fredrick Shija wakati akizungumza katika maadhimisho hayo yaliyofanyika kata ya Mwitikira Wilaya ya Bahi Mkoani Dodoma.
Shija amesema maadhimisho ya siku ya mtoto wa Afrika inawakumbusha wazazi na walezi haki za mtoto ambapo ni wajibu wa kila mmoja kumlinda mtoto na kuhakikisha anapata haki zake zote za msingi.
"Siku hii ni muhimu kwa ajili ya kukumbusha wajibu wa wazazi kwa watoto wao"Amesema Shija.
Amesema serikali isimamie uanzishwaji wa mabaraza ya watoto Nchini ili iwe rahisi kujua madhila wanayokutana nayo na kujua changamoto wanayokutananayo.
Akizungumza katika maadhimisho hayo kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Bahi, Katibu Tawala Bi.Mwanamvua Bakari amewataka wazazi na walezi kutimiza wajibu wao kwa watoto ili waweze kutimiza ndoto zao.
Aidha ameitaka jamii kushirikiana na Serikali pamoja na wadau katika kuwalinda watoto na kuwatimizia mahitaji yao.
"Watoto Hawa ndio viongozi waheshimiwa wa kesho,tuwalinde na kuwatunza "Amesema Mwanamvua.
Mmoja wa wanafunzi kutoka shule ya sekondari Chiboli Gift Mdoya amesema serikali iwekeze kwa watoto kwa maendeleo Endelevu kwa kuweka miundombinu Bora ya elimu ili watoto waweze kutimiza ndoto zao hasa wanaokaa vijiji wajengewe shule karibu ili kuondoa umbali mrefu.
"Serikali iweke mazingira Bora ya kujifunzia,kujenga mabweni na kuwe na Ongezeko la shule karibu na makazi ili kupunguza umbali hasa kwa watoto waishio vijijini pamoja na Ujenzi wa Maabara"Amesema Gift.
Fedilis Kasota mwanafunzi wa darasa la saba kutoka shule ya msingi mwitikira amewaomba wazazi na walezi wawasimamie watoto na kutoa mahitaji ili waweze kutimiza maono yao.