Na Avelina Musa - Dodoma.
MKURUGENZI Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa huduma za Nishati na Maji (EWURA) Dkt.James Andilile amewataka Watanzania kutumia wiki ya utumishi wa Umma kama jukwaa la kupata taarifa mbalimbali za EWURA na kueleza kuwa hali hiyo itaboresha mifumo ya utoaji huduma na kujifunza kutoka kwa wadau na wananchi.
Katika kipindi cha wiki ya utumishi wa umma, EWURA imekuwa ikikutana moja kwa moja na wananchi ili kusikiliza changamoto, kutoa elimu kuhusu haki na wajibu wao, na kueleza namna taasisi hiyo inavyosimamia bei, ubora, na upatikanaji wa huduma za mafuta, umeme, gesi asilia, na maji safi na usafi wa mazingira.
Dkt.Andilile amesema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari katika maadhimisho ya wiki ya Utumishi wa Umma yanayoendelea katika viwanja vya Chinangal Park Jijini Dodoma ambapo amesema EWURA inatambua kwamba huduma bora kwa umma ni chachu ya ustawi wa jamii na uchumi wa nchi, hivyo itaendelea kusimamia misingi ya utawala bora uwazi na uwajibikaji.
Amesema kumekuwa na maboresho katika mifumo ya TEHAMA ambayo yamewezesha wananchi kupata huduma wakiwa mahali popote Nchini bila kufika katika Ofisi za Mamlaka hiyo kwani huduma zote zinapatikana mtandaoni kupitia mifumo ya kidijitali.
"Tumejipanga kuhakikisha wananchi hawapotezi muda kusafiri kwenda Ofisi za EWURA ambapo kwa sasa huduma zote zinapatikana kwa njia ya mtandao katika mifumo yetu ya kidijitali,"Amesema Andilile.
Wiki ya Utumishi wa Umma huadhimishwa kila mwaka kwa lengo la kuhamasisha uwajibikaji, maadili ya kazi, pamoja na kutoa nafasi kwa taasisi za umma kusikiliza na kutatua changamoto zinazowakabili wananchi katika upatikanaji wa huduma.
EWURA ni miongoni mwa taasisi za Serikali zinazoshiriki katika maadhimisho ya wiki ya Utumishi wa Umma kwa mwaka 2025 ikiwa ni sehemu ya juhudi za serikali katika kuboresha uwajibikaji na utoaji wa huduma Bora kwa wananchi.