WIZARA YA KATIBA NA SHERIA YATOA ELIMU YA MSAADA WA KISHERIA BURE WILAYANI BAHI.

MUUNGANO   MEDIA
0

 



Na Avelina Musa - Dodoma.


KATIKA kuhitimisha Kongamano la Jukwaa la Mashirika yasiyo ya Kiserikali,Wizara ya Katiba na Sheria yatoa elimu ya msaada wa kisheria bure kupitia kampeni ya Mama Samia Legal Aid  katika ngazi ya Kata Wilayani Bahi.

Ambapo  imetoa elimu ya msaada wa Kisheria Bure na kusikiliza kero mbali mbali kutoka kwa wananchi wa Kata ya Mpinga na  Kijiji cha Nagulo Wilayani Bahi.

 Kaimu Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Bahi Mhe.Joyce Manyanda  ameipongeza Wizara ya Katiba na Sheria kwa kuendelea kutoa elimu ya Sheria kwa wananchi kupitia kampeni ya Mama Samia Legal Aid na kuahidi kutoa ushirikiano kwa wataalam hao.




Akizungumza na wananchi wa Kata ya  Mpinga Wakili wa Serikali Kasilida Chimagi   kutoka Wizara ya Katiba na Sheria amesema lengo la kutoa Elimu hiyo  ni kupunguza migogoro katika Jamii ili kuwafanya wananchi waelekeze nguvu zao katika shughuli za Kimaendeleo.



Amesema  wanategemea baada ya Elimu hiyo kutolewa  migogoro itapungua au kuisha kabisa na jamii itaishi kwa utulivu na kuelekeza nguvu zao katika uzalishaji wa mali.

Akitoa Mada inayohusu Ukatili wa kijinsia Msaidizi wa Kisheria kutoka Jicho Angavu Foundation Husein Mikulu amesema kumekuwa na changamoto ya tamaa katika jamii linalopelekea kutokea kwa vitendo vya ukatili wa kijinsia kwa watoto na wanawake kama ndoa za utotoni na wanawake kutokumiliki mali.

 

"Mtoto wa kike  kukatizwa kielimu na kuozeshwa bila kutimiza ndoto zake huo ni ukatili wa kijinsia"Amesema Mikulu.

Mikulu amewaasa wazazi na walezi kuwalinda watoto dhidi ya ukatili wa aina yeyote ikiwemo Ushoga na ulawiti pamoja na kutimiziwa haki zote za msingi bila Ubaguzi.

"Kumekuwa na ukatili kwenye ndoa katika kumiliki Mali Kuna jamii haziruhusu mke amiliki mali."Amesema.

Akitoa Elimu kwa wanafunzi wa shule ya msingi Mpinga Afisa Sheria,Sheria ya Mtoto,Haki na Wajibu wa mtoto kutoka Wizara ya Katiba na Sheria Sr.Winifrida Masiaga amesema watoto wanapaswa kujua haki zao zote na watimiziwe bila kubughudhiwa.

Hata hivyo baadhi ya wananchi wa kata ya Mpinga Gaitani  Selemani na Henry Singo  wameiomba  Wizara ya Katiba na Sheria kuweka mawakala wa msaada wa kisheria katika kila Kata ili wapate huduma kwa wakati.




Kwa Upande wake Mwenyekiti wa Kijiji cha Mpinga Hezron Mbeyo  ameipongeza Wizara ya Katiba na Sheria kwa kufika katika Kijiji hicho na Kata hiyo kutoa elimu  kwani wamekuwa na kero ya mara Kwa mara ya migogoro ya Ardhi na ndoa.


 






Chapisha Maoni

0Maoni
Chapisha Maoni (0)