Na Avelina Musa - Dodoma.
MAMLAKA ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) imewaita wakazi wa Dodoma kujitokeza kwa wingi kufika katika maonesho yanayoendelea katika viwanja vya Chinangal Park Jijini Dodoma kuhusu majukumu yake pamoja na fursa lukuki zinazopatikana katika sekta ya mafuta na gesi asilia, hasa mkondo wa juu wa petroli.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Kitengo cha Ushirikishwaji wa Wazawa na Ushirikiano wa Ndani, Bw. Charles Nyangi wakati akizungumza na waandishi wa habari katika banda la PURA kwenye maonesho hayo,ambapo amesema PURA ilianzishwa kwa mujibu wa Sheria ya Petroli ya mwaka 2015, likiwa na jukumu la kusimamia na kudhibiti shughuli zote za utafutaji na uzalishaji wa mafuta na gesi asilia nchini.
“Majukumu yetu muhimu ni kuhamasisha ushiriki wa wazawa kwenye shughuli za mkondo wa juu wa petroli ambapo Ushiriki huu umegawanywa katika maeneo matatu makuu kupitia ajira, kupitia ujasiriamali kwa maana ya utoaji wa bidhaa kupitia uwekezaji,”Amesema Nyangi.
Bw.Nyangi amesema kushiriki kwa PURA katika maonesho hayo kunalenga kuwaelimisha wananchi juu ya majukumu ya mamlaka na namna wanavyoweza kushiriki kikamilifu katika sekta hiyo muhimu ya kiuchumi.
Amesema kupitia usimamizi wa PURA, Serikali inalenga kuhakikisha kuwa rasilimali za mafuta na gesi asilia zinawanufaisha Watanzania wote kwa kuimarisha ushirikishwaji wa wazawa, kukuza ujuzi wa kitaifa na kuongeza fursa za kiuchumi.
Aidha, amesema gesi asilia imekuwa na mchango mkubwa katika maendeleo ya taifa, hasa kwenye sekta ya uzalishaji wa umeme na uwekezaji wa Serikali katika miradi ya umeme wa bwawa ambayo inachangia kuongeza upatikanaji wa nishati endelevu.
“Gesi hii ni muhimu kwa matumizi ya majumbani, viwandani, na sasa tunasonga mbele kuhakikisha inatumika pia kwenye magari ambapo tayari gesi inapatikana Mtwara, Lindi na Dar es Salaam na Serikali inaendelea kuwekeza ili kusambaza huduma hiyo katika mikoa mingine,”Amesema.