WIZARA YA MADINI IMELIOMBA BUNGE KURIDHIA NA KUPITISHA BAJETI YA BILION 224.

MUUNGANO   MEDIA
0

 



Na Avelina Musa - Dodoma.

Wizara ya Madini imeliomba Bunge kuridhia na kupitisha makadirio ya bajeti ya Shilingi Bilioni 224,984,150,000.00 kwa ajili ya matumizi ya Wizara na Taasisi zake kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026.

Akiwasilisha bajeti hiyo  leo Mei 2,2025 Bungeni Jijini Dodoma Waziri wa Madini Mhe,Anthony Mavunde,amesema  Serikali inaendelea kuchukua hatua za kimkakati ili kuvutia uwekezaji wa ndani na nje katika sekta ya Madini nchini.
Mhe, Mavunde amevitaja vipaumbele vya wizara kuwa  ni  kuongeza mchango wa Sekta ya Madini kwenye Pato la Taifa,kuendeleza mnyororo wa thamani katika madini muhimu na madini mkakati.
“Kuhamasisha uwekezaji na uongezaji thamani madini,kuimarisha uendeshaji wa minada na maonesho ya madini ya vito,kuongeza uwekezaji kwenye tafiti za madini za kina, kurasimisha”amesema Mavunde
Vipaumbele vingine ni kuendeleza wachimbaji wadogo wakiwemo vijana, wanawake na watu wenye ulemavu  na kuzijengea uwezo taasisi zilizo chini ya wizara ya madini.

Kati ya fedha hizo, shilingi bilioni 24,268,585,000.00 ni kwa ajili ya mishahara ya watumishi (PE) na shilingi bilioni 76,110,777,000.00 kwa ajili ya matumizi mengineyo (OC) ya Wizara na Taasisi zilizo chini yake.

Aidha,amesema Tanzania imeendelea kuchukua hatua za kuimarisha biashara ya almasi kwa kuanzisha minada, maonesho, masoko na kuhamasisha uwekezaji katika uchakataji wa madini ya almasi ndani ya nchi.

" Mheshimiwa Spika, napenda kulifahamisha Bunge lako Tukufu kwamba Tanzania ni miongoni mwa nchi zilizobarikiwa kuwa na madini mkakati na madini muhimu (strategic and critical minerals) ambayo yanazidi kuhitajika duniani kwa ajili ya matumizi katika teknolojia za kisasa na nishati mbadala, " Amesema 

Hata hivyo ameeleza kuwa mahitaji ya madini haya, yakiwemo lithium, cobalt, nickel, copper, aluminium, zinc, graphite, na rare earth elements (REE), yameendelea kuongezeka kutokana na jitihada za kimataifa za kupunguza hewa ya ukaa ifikapo mwaka 2050 (Net Zero Emission). 

Amesema Kuongezeka kwa mahitaji haya kunatokana na kuongezeka kwa uzalishaji wa magari ya umeme, betri za kuhifadhi nishati, na vifaa vya teknolojia ya kisasa vikiwemo simu janja, darubini na kompyuta. 

"Mheshimiwa Spika, hali hii inatoa fursa kubwa kwa Tanzania kuhakikisha madini haya yanaongezwa thamani ndani ya nchi ili kuongeza mapato, ajira, na mchango wake katika uchumi wa Taifa," Amesema

           Mwisho.






Chapisha Maoni

0Maoni
Chapisha Maoni (0)