Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa amefunga Maonesho ya Wiki ya Nishati katika Viwanja vya Bunge jijini Dodoma na kutoa maagizo kwa
Wizara ya Nishati na Taasisi zake kuendelea kuboresha maonesho hayo na utoaji wa huduma kwa wananchi.
Mhe. Majaliwa ameitaka Wizara ya Nishati kuweka mkakati wa kuhakikisha maonesho hayo yanakuwa endelevu ili wabunge wapate fursa za
kuwasilisha hoja zao moja kwa moja kwa wataalam na kupewa majawabu ya hoja na changamoto zinazowakabili wao na wananchi wanaowakilishwa.
Aidha, ameagiza Maonesho ya Nishati yafanyike kuanzia ngazi ya wilaya, mikoa na halmashauri ili yale yanayofanyika Makao Makuu yabaki kuwa ya
Kitaifa.
Amefafanua kuwa kwa kufanya hivyo huduma zitakuwa zimesogezwa zaidi
kwa kwa wananchi na pia Mameneja wa TANESCO wa Kanda, Mikoa na Wilaya watoe ufafanuzi wa hoja na changamoto zinazowakabili wananchi husika.
Vilevile ameitaka Wizara kuweka mkakati wa kuwawezesha wananchi wote kupata ufafanuzi na fursa zinazotokana na miradi inayotekelezwa katika
Sekta ya Nishati.
Aidha,katika hatua nyingine, Waziri Mkuu ametoa agizo kuwa Taasisi zote
zinazolisha watu wengi kuanzia 50 hadi 100 waanze kubadilisha
teknolojia ya kupikia na kutumia Nishati Safi ya Kupikia na ifikapo
mwisho wa mwaka 2024 Serikali inataka kuona asilimia 99 ya Taasisi za aina hiyo zinatumia Nishati Safi ya Kupikia.
Vilevile amempongeza Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati kwa
utendaji kazi wake ambao umechochea hali ya upatikanaji umeme nchini kuongezeka na kutosheleza mahitaji na pia kuwezesha upatikanaji wa
umeme wa ziada.
Kwa upande wake, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Doto Biteko amelipongeza Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kwa kuendelea
kuboresha utoaji huduma ya umeme nchini.
Amesema, “ tunafanyakazi kubwa kubadilisha taswira ya Wizara ya
Nishati na Taasisi zake na niwashukuru sana watendaji wa Wizara hii na Taasisi zake kwa kufanyakazi kwa juhudi na niwaombe waongeze kasi.”
Amesema Dkt. Biteko.
Amewapongeza wakandarasi wa umeme kwa kuendelea na utekelezaji wa miradi ya nishati katika maeneo mbalimbali nchini, sambamba na kuvipongeza vyombo vya habari nchini kwa kuendelea kutangaza habari
zinazohusu masuala ya nishati kwa lengo la kujibu hoja na maswali
mbalimbali ya wananchi.
Kwa upande wake, Spika wa Bunge Mhe. Dkt. Tulia Ackson, amesema kuwa sekta ya nishati ni moja kati ya sekta mtambuka nchini inayochagiza
maendeleo ya Sekta nyingine na kwamba ili maendeleo yapatikane sekta ya nishati ina mchango mkubwa.
Mwisho.