STORIA imeandikwa kwa mara ya kwanza baada ya Shirika la Reli Tanzania(TRC) kuzindua njia ya Reli ya kisasa (SGR) kuanzia Dar es Salaam-Dodoma ikiwa ni sehemu ya mafanikio ya miaka 60 ya Muungano.
VIONGOZI wa Dini kutoka madhehebu mbalimbali wamewasili jijini Dodoma kwa ajili ya kuliombea Taifa kwa kutumia treni ya kisasa inayotumia umeme ya majaribio kutoka Dar es Salaam.
Akizungumza mara baada ya kuwapokea viongozi hao jijini hapa leo,Aprili 21,2024,Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Dkt.selemani Jafo akiwa na viongozi wengine mbalimbali akiwemo Mkuu wa Mkoa wa Dodoma,Rosemary Senyamule pamoja na wananchi amesema kuwa viongozi hao wanatarajiwa kushiriki ibada maalum ya kuliombea Taifa katika uwanja wa Jamhuri leo Aprili 22,2024 wakiongozwa na Makamu wa Rais Dkt.Philip Mpango.
Waziri Dkt.Jafo amesema kuwa wakati taifa linaelekea kuadhimisha miaka 60 ya Muungano suala la viongozi wa dini kusafiri kwakutumia treni ya kisasa ya umeme ni mafanikio makubwa na serikali imeona ni vyema viongozi wa dini kuwa wa kwanza kusafiri na usafiri huo wakiwa wanaenda kuliombea Taifa.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu Shirika la Reli Tanzania(TRC)Masanja Kadogosa amesema kuwa wanaposafiri na treni hiyo wanatesti madaraja kuhakikisha ubora wake upo vizuri pamoja na makalavati.
Aidha amesema kuwa Treni hiyo ya umeme iliyobeba watu mbalimbali pamoja na viongozi wa dini 160 imetumia umeme wa shilingi milioni 1.2 kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma kwa saa 3 na dakika 21.
Mwisho.