Serikali imezielekeza Mamlaka za Serikali za Mitaa kutekeleza jukumu lao la
kuhakikisha taka zote katika maeneo yao zinakusanywa na kutupwa katika
madampo yaliyopo.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na
Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo wakati akichangia taarifa ya utekelezaji ya
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira bungeni jijini Dodoma.
Amesema kuwa kila halmashauri nchini ni lazima iweke utaratibu mzuri wa
zoezi la uzoaji wa taka ngumu na si kuziacha zikizagaa ovyo kwenye mitaa hali
inatoweza kusababisha magonjwa.
“Nashukuru kuna yale madampo matano yaliyojengwa katika mikoa
mbalimbali kupitia mradi lakini baadhi ya halmashauri bado zinasuasua katika
ukusanyaji wa taka..utakuta mtu amepewa tenda (zabuni) halafu hilo lori
lenyewe analotumia ni takataka, hili haliwezekani lazima tufikie mahali
tutumizi majukumu yetu,“ amesema.
Dkt. Jafo ameongeza kuwa Ofisi ya Makamu wa Rais jukumu lake ni
kusimamia sera wakati halmashauri hizo zinapaswa kutekeleza jukumu lao la
kuhakikisha maeneo yao yanakuwa safi.
Akiendelea kuchangia hoja hiyo, alielekeza kuwa majengo yote yanayojengwa
hasa katika majiji ni lazima yawe na mifumo ya uvunaji wa maji hatua
itakayosaidia kupunguza uharibifu wa miundombinu ya majitaka.
Alisema kuwa miundombinu ya majitaka hasa mifereji inapoharibika
husababisha uchafu kukwama badala ya kwenda kwenye mabwawa ya
majitaka na hivyo kusababisha mafuriko.
Kwa upande mwingine Waziri Dkt. Jafo alisema kuwa mchakati wa uhuishaji
wa Sheria ya Mazingira ya mwaka 2004 namba 191 upo katika hatua nzuri na
unatarajiwa kukamilika mwaka huu.
Alisema kuwa ni kweli sheria hiyo ina mambo mengi yanayotakiwa kuhuishwa
na ni lazima iende na wakati sanjari na Sera ya Taifa ya Mazingira ya mwaka
2021 ili ikidhi haja.
Hivyo, Waziri Dkt. Jafo alifafanua kuwa Sheria ya Mazingira inayohuishwa
imegusa mambo mengi ya msingi yakiwemo mchakato wa kulipa nguvu
Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kuwa mamlaka
kamili na kukiimarisha Kituo cha Ufuatiliaji wa Kaboni (NCMC).
Awali akiwasilisha taarifa ya kamati hiyo, Mwenyekiti wake Mhe. Jackson
Kiswaga alisema katika kuhakikisha ukakatiji wa miti unapungua au kuisha
kabisa Bunge linaishauri Serikali kuweka ruzuku katika gesi ili wananchi wawe
na uwezo wa kumudu kutumia nishati hiyo ambayo rafiki kwa mazingira.
Halikadhalika alisema Bunge linaitaka Serikali kuchukua hatua madhubuti
kuhakikisha mchakato wa kuhuisha Sheria ya Mazingira namba 191
unakamilika, ambao unatarajiwa kukamilika mwaka 2024.
Aidha, Mhe. Kiswaga ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Kalenga alitoa
ushauri kwa Serikali iweke mwongozo kwa magari yanayobeba taka ngumu
kuyafunika ili zisianguke na kuchafua mazingira.
Kwa upande wake Mbunge wa Viti Maalumu Mhe. Regina Qwaray aliiomba
Serikali isimamie kanuni na miongozo ya mazingira kukabiliana na wale
wanachafua mazingira.
Pia, Mbunge huyo aliipongeza Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kusimamia vyema
katazo la matumizi ya mifuko ya plastiki na kuhimizi viwanda viendelee na
shughuli ya urejelejezaji wa chupa za plastiki hatua itakayosadia zisizage ovyo
na kuchafua mazingira.
Alitahadharisha pia kuhusu uchimbaji wa mchanga na kokoto unafanyika
kiholela kwenye makazi ya watu yanatokea na kusababisha makorongo
ambayo hufanya mmomonyoko wa ardhi unaosababisha mafuriko.

.jpg)