Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip
Mpango amesema jitihada inahitajika katika kutoa elimu ya magonjwa
yasioambukiza pamoja na kuzingatia mtindo bora wa maisha, mazoezi na
kufanya vipimo vya afya mara kwa mara ili kukabiliana na maradhi mbalimbali
ikiwemo magonjwa ya moyo.
Makamu wa Rais amesema hayo wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa
Kimataifa wa Magonjwa ya Moyo unaofanyika katika Ukumbi wa Golden Tulip
Airport – Unguja, Zanzibar. Amesema katika kukabiliana na ugonjwa wa moyo
ni muhimu wananchi kufuata njia za kujikinga zaidi ikiwemo kuacha ulevi
uliyopindukia, uvutaji sigara, tabia bwete pamoja na uzito uliyopindukia.
Ametoa rai kwa watalaamu wa afya, wasomi, vyombo vya habari pamoja na
watunga sera kushiriki katika utoaji elimu kuhusu masuala ya afya.
Aidha Makamu wa Rais amesema tafiti zinapaswa kufanyika kwa kina ili
kubaini visababishi zaidi vya magonjwa ya moyo kwa kupata taarifa zaidi juu
ya taratibu za kijamii na tabia za kiutamaduni katika mambo mbalimbali
yaliyozoeleka kufanyika barani Afrika.
Makamu wa Rais amesema Tanzania imechukua hatua mbalimbali katika
kukabiliana na magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo magonjwa ya moyo kama
vile kuimarisha Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete, kufanya tafiti za afya za
kimkakati ili kupata suluhu ya changamoto mbalimbali za kiafya zinazowakabili
wananchi pamoja na kutoa elimu ya magonjwa yasiyoambukiza na magonjwa
adimu.
Amesema Taasisi ya Moyo ya jakaya Kikwete imeendelea kuimarika ambapo
kwa sasa inafanya upasuaji kwa wagonjwa wa moyo 800 kwa mwaka ikiwemo
upausaji wa kufungua kifua (upasuaji mkubwa) ukilinganisha na wagonjwa
200 wakati ikianzishwa. Amesema zaidi ya wagonjwa laki mbili hutibiwa kwa
mwaka huku zaidi ya 2400 wakitoa mataifa mengine. Ameongeza kwamba
serikali imeweza kuokoa zaidi ya bilioni 63 kila mwaka za matibabu ya
wagonjwa wa moyo kutokana na kuimarishwa kwa Taasisi ya Moyo ya Jakaya
Kikwete.
Vilevile Makamu wa Rais amesema serikali itaongeza uwekezaji katika huduma
za magonjwa ya moyo na kuandaa mipango ya awali, ubunifu, tafiti ,
mafunzo, ushirikiano, udhibiti na utoaji tiba wa magonjwa ya moyo nchini.
Mkutano huo wa siku mbili uliyoandaliwa na Taasisi ya Moyo ya Jakaya
Kikwete unawakutanisha Madaktari Bingwa, wataalam na wadau wa afya,
wauguzi na watunga sera kutoka mataifa zaidi ya 40 duniani kwa lengo la
kujadiliana na kubadilishana uzoefu katika masuala mbalimbali yanayohusu
magonjwa ya moyo duniani.
Imetolewa na
Ofisi ya Makamu wa Rais
09 Februari 2024
Zanzibar.

