Bodi ya Nishati Vijijini (REB) inayosimamia Wakala wa Nishati Vijijini
(REA), imesema inategemea mafanikio makubwa katika kuiwezesha
Wakala hiyo kutimiza azma yake ya kuwafikishia wananchi walioko vijijini
nishati bora za umeme, mafuta na gesi.
Hayo yamebainishwa mwishoni mwa wiki na Mwenyekiti wa Bodi hiyo,
Balozi, Meja Jenerali Mstaafu, Jacob Kingu baada ya kikao cha kwanza
cha Bodi hiyo mpya kilicholenga kutambuana na kupanga majukumu.
“Kikao chetu kimeenda vizuri, tumechagua Kamati na kupangiana
majukumu. Tunaamini na tunaahidi kuwa tutatekeleza majukumu yetu
sawasawa na Sheria iliyoanzisha Wakala wa Nishati Vijijini inavyoelekeza,”
amesema.
Aidha, Balozi Kingu amemshukuru Mheshimiwa Rais Samia Suluhu
Hassan kwa kumteua kuwa Mwenyekiti wa Bodi na amemshukuru Naibu
Waziri Mkuu ambaye pia ndiye Waziri wa Nishati, Mheshimiwa Dkt. Doto
Mashaka Biteko kwa kukamilisha mchakato wa uteuzi wa Wajumbe wa
Bodi, jambo ambalo limeiwezesha kuwa Bodi kamili.
Akieleza zaidi kuhusu majukumu waliyojipangia, Balozi Kingu amesema
mapema Mwezi Machi, Bodi itakutana katika kikao cha dharura kupitia na
kujadili masuala mbalimbali ya Wakala ambayo yalikuwa yakisuburi baraka
za Bodi ili kuyatolea maamuzi yatakayowezesha utekelezaji wake kwa
manufaa ya wananchi na Taifa kwa ujumla.
Kwa upande wake, Katibu wa Bodi hiyo ambaye pia ni Mkurugenzi wa
REA, Mhandisi Hassan Saidy amepongeza Mamlaka za Uteuzi, kuteua
watu makini, hodari na wachapakazi ambao amesema ni muhimu kuwa
nao katika kuisimamia Wakala hiyo yenye majukumu makubwa
yanayogusa maisha ya wananchi moja kwa moja.
“REA ina jukumu kubwa ambalo linagusa maisha ya watu lakini pia
linahusisha kiasi kikubwa sana cha fedha za Serikali. Kwahiyo, kuwa na
Bodi nzuri iliyosheheni watu makini, kwetu sisi ni jambo la faraja,”
amefafanua.
Mkurugenzi Mkuu, kwa niaba ya Menejimenti na Wafanyakazi wote wa
REA, ametoa ahadi ya ushirikiano kwa Bodi hiyo mpya ili kuhakikisha
malengo ya Serikali kupitia majukumu yaliyokasimiwa kwa Wakala
yanatekelezwa.
“Tunatamani kuona Watanzania wenzetu wanaoishi vijijini wanapata nishati
bora kama ilivyo kwa wenzao wanaoishi mjini,” amesisitiza.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, Wajumbe wa Bodi wamezishukuru
Mamlaka za Uteuzi kwa kuwaamini na kuwapa jukumu hilo kubwa la
kuisimamia REA ili kuendelea kuleta matokeo chanya.
Aidha, wamepongeza Bodi zilizotangulia kabla yao, Menejementi pamoja
na Wafanyakazi wote kwa kazi nzuri waliyofanya tangu kuanzishwa kwa
Wakala na kuahidi kuendeleza yote mazuri yaliyofanyika ili kuongeza tija.
Kikao hicho pia kilishirikisha Menejimenti ya Wakala ambapo Wakuu wa
Idara na Vitengo waliwasilisha kwa Bodi taarifa za utekelezaji wa
majukumu katika maeneo wanayosimamia kwa lengo la kuijengea Bodi
uelewa na ufahamu kuhusu Taasisi hiyo waliyopewa jukumu la kuisimamia.
Januari 26 mwaka huu, Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa
Nishati, Dkt. Doto Biteko aliwateua Florian Otman Haule, Lucas Charles
Malunde, Mwantum Issa Sultan, Stephen Menard Mwakifamba, James
Issack Mabula, Ahmed Martin Chinemba, Sophia Shaban Mgonja na Balozi
Radhiya Naima Msuya kuwa Wajumbe wa Bodi ya Nishati Vijijini,
wakiungana na Balozi Meja Jenerali Mstaafu Jacob Gideon Kingu
aliyeteuliwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan, Septemba 2023
kuwa Mwenyekiti wa Bodi hiyo.
CAPTIONS
PIC 1
Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB), Balozi, Meja Jenerali Mstaafu
Jacob Gideon Kingu (katikati-waliokaa), akiwa katika picha ya pamoja na
Wajumbe wapya wa Bodi hiyo baada ya kikao chao cha utambulisho na
kupanga majukumu kilichofanyika hivi karibuni katika Ofisi Ndogo za
Wakala wa Nishati Vijijini (REA) zilizopo jijini Dar es Salaam.
PIC 2
Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB), Balozi, Meja Jenerali Mstaafu
Jacob Gideon Kingu (katikati-waliokaa) na Wajumbe wapya wa Bodi hiyo,
wakiwa katika picha ya pamoja na Menejimenti ya Wakala wa Nishati
Vijijini (REA) baada ya kikao chao cha utambulisho na kupanga majukumu
kilichofanyika hivi karibuni katika Ofisi Ndogo za REA zilizopo jijini Dar es
Salaam.

