Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt. Philip Mpango
ametoa wito kwa washiriki wa Kongamano la lugha za asili kujielekeza katika
kupanga mikakati itakayohakikisha Kiswahili na lugha nyingine za asili zinapata
fursa katika uchumi wa kidijiti ili kuwawezesha wananchi kushiriki kikamilifu katika
sekta hiyo.
Makamu wa Rais amesema hayo wakati wa ufunguzi wa Kongamano la Kimataifa
la Dhima ya Lugha za Asili katika kuendeleza Diplomasia ya Kiuchumi na
Kiutamaduni lililofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Four Points by Sheraton
Jijini Dar es salaam. Amesema Kongamano hilo linapaswa kuangazia namna
ambavyo Kiswahili pamoja na lugha nyingine za asili za Afrika zitakavyotumika
kuendeleza teknolojia za asili, kuchochea uvumbuzi, uwekezaji na kukua kwa
diplomasia.
Aidha Makamu wa Rais amesema Kongamano hilo linapaswa kusaidia kuonesha
fursa zilizopo katika matumizi ya lugha za asili ili kuwafanya vijana kujipatia stadi
na maarifa mbalimbali katika kujiandaa kwa mabadiliko makubwa ya kiuchumi na
kiteknolojia ndani na nje ya bara la Afrika.
Makamu wa Rais amesema kupitishwa kwa Kiswahili kuwa lugha rasmi katika
Umoja wa Afrika (AU) na Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika
(SADC), kumepanua wigo wa matumizi ya Kiswahili na kuleta fursa mbalimbali za
kiuchumi na kiutamaduni. Amesema Kongamano hilo ni muhimu kubeba jukumu
kubwa la kuibua fursa zaidi na kuendeleza historia ndefu ya Kiswahili katika
kujenga uhusiano kati ya watu wa tamaduni, lugha na misingi mbalimbali ya
kiuchumi na kijamii.
Amesema Katika muktadha wa ukuaji na maendeleo ya Kiswahili, ikiwa ni pamoja
na kuhifadhi lugha nyingine za asili, tamaduni na mifumo ya maarifa asili, katika
Afrika Mashariki na Kati, wafanyabiashara wadogo na wanaoinukia
“Wamachinga” wametoa mchango ambao hauna budi kutambuliwa na
kuthaminiwa. Amesema lipo hitaji la kufanya utafiti wa kina ili kuona jinsi nchi za
Kiafrika zinavyoweza kuendeleza mifumo inayozingatia ushiriki wa vijana na
makundi kama ya wafanyabiashara waliojiajiri katika diplomasia ya kiuchumi na
kukuza biashara.
Halikadhalika Makamu wa Rais amesema Tanzania imeweka kipaumbele katika
kukuza lugha ya Kiswahili, ambapo inalenga kuifanya lugha hiyo kuendelea kuleta
umoja, amani na kuvumiliana katika bara zima la Afrika. Amekipongeza Chuo
Kikuu cha Dar es Salaam kwa kuendelea kushirikiana na Vyuo na Taasisi za nje
katika kukuza Kiswahili na kuendeleza diplomasia ya kiutamaduni.
Kongamano hilo limehudhuriwa na Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Msumbiji Mhe.
Joackim Chissano, Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Kenya Mhe. Uhuru Kenyatta,
Wanadiplomasia, Watunga sera, Wafanyabiashara na wenye Viwanda, Viongozi
wa Dini, Wanataaluma na Wakuu wa Taasisi za Utafiti, Vijana, Wanawake na
wawakilishi wa mashirika mbalimbali ya kiraia. Kongamano limeandaliwa na Chuo
Kikuu Cha Dar es salaam kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Kwazulu Natal cha
Afrika Kusini
Imetolewa na
Ofisi ya Makamu wa Rais
20 Februari 2024
Dar es salaam.

.jpg)