Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis
Hamza Khamis amewahimiza wasimamizi wa miradi kwenye halmashauri
kuendelea kuisimamia vyema ili ilete tija kwa wananchi.
Amesema hayo wakati wa Ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na
Mazingira ilipotembelea na kukagua Mradi wa Kuhimili Mabadliko ya Tabianchi
kwa kutumia Mifumo Ikoklojia Vijijini (EBARR) katika Halmashauri ya Wilaya ya
Mpwapwa mkoani Dodoma.
Mhe. Khamis amesema kuwa ni muhimu kwa wasimamizi hao kusimamia
vyema fedha zinazoletwa na Serikali kwa ajili ya kutekeleza miradi hiyo, hivyo
kuleta matokeo tarajiwa na kuwanufaisha walengwa.
Pia, amewataka wananchi walionufaika na miradi hiyo kuitunza ili idumu hatua
itakayosaidia kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi zinazoyakabili
meneo kadhaa nchini na duniani kwa ujumla.
Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya
Maji na Mazingira Mhe. Anna Lupembe ametoa pongezi kwa Ofisi ya Makamu
ya Rais kwa utekelezaji mzuri wa mradi huo.
Mhe. Lupembe ametoa wito kwa wananchi kuzungumzia mazuri yanayofanywa
na Serikali katika kutekeleza miradi hii mikubwa ambayo imewatatulia
changamoto zao.
“Tuipongeze Serikali ya Rais wetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan
kwani imewakomboa wananchi kwa kuwatua wanawake ndoo kichwani na
kuwawezesha kujipatia kipato kupitia mradi huu wa maji na kitaku nyumba
tukichotembelea,” amesema.
Miradi ilitembelewa na Kamati ni pamoja na mashine ya kukamua mafuta ya
alizeti na kliniki ya mifugo katika Kijiji cha Ngh’ambi, josho la kuogeshea
mifugo na kisima pamoja na kitaku nyumba katika Kijiji cha Kazania.
Mradi wa EBARR unatekelezwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu
(Shinyanga), Mvomero (Morogoro), Mpwapwa (Dodoma), Simanjiro (Manyara)
kwa upande wa Tanzania Bara na kwa upande wa Tanzania Zanzibar
unatekelezwa katika Wilaya ya Kaskazini A, Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Kupitia mradi huu wananchi wanajengewa uwezo wa kuhimili changamoto za
mabadiliko ya tabianchi kwa kuimarisha uwezo wao wa uvumilivu na uwezo
wa mifumo ikolojia inayowazunguka kusaidia katika kuhimili athari za
mabadiliko ya tabianchi.
