Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip
Mpango amesema ili kukabiliana na changamoto za utengenezaji ajira barani
Afrika yanahitajika mageuzi na mbinu jumuishi kwa kuimarisha ushirikiano
baina ya wadau wote husika.
Makamu wa Rais ametoa wito huo wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa 7 wa
Wadau wa Kijamii wa Afrika katika masuala ya Kazi na Ajira uliyofanyika
katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere Jijini Dar es
salaam, tarehe 07 Februari 2024. Amesema linahitajika jukwaa la utekelezaji
litakalounganisha mashirika ya serikali, washirika wa ndani ya nchi, sekta
binafsi pamoja na wadau wa kimataifa ili kukabiliana na changamoto za
utengenezaji wa ajira.
Makamu wa Rais amesema nchi za Afrika zinapaswa kuongeza ujuzi na
matumizi ya teknolojia ili kuongeza tija katika uzalishaji badala ya kuona
teknolojia ni adui kwa usalama wa ajira. Amesema ujio wa Akili Mnemba
(Artificial Intelligence) utaathiri utengenezaji wa ajira kwa kupunguza ajira
ndogondogo zilizopo na kutengeneza ajira mpya hususani zinazohitaji ujuzi wa
kiufundi.
Makamu wa Rais amesema matumizi ya Akili Mnemba yanazitaka Serikali na
sekta binafsi katika bara la Afrika kutoa kipaumbele kwa kuwapa wafanyikazi
ujuzi wa juu zaidi wa kiteknolojia ili kuwawezesha kuendana na soko jipya la
ajira. Ametoa wito kwa Mkutano huo kujadili umuhimu wa mafunzo mapya
kwa wafanyakazi, kufanya uchambuzi, kutambua sekta ambazo zina
uwezekano wa kupoteza idadi kubwa ya fursa za ajira na sekta ambapo Akili
Mnemba itaongeza ajira za ujuzi wa juu. Amesema eneo moja mahususi
ambalo Akili Mnemba inaweza kusaidia kutengeneza ajira ni utafiti wa kilimo
unaolenga kuboresha aina za mbegu zenye mavuno mengi na mbegu
zinazostahimili ukame ambazo zitachochea tija kubwa na ajira za baadaye.
Halikadhalika Makamu wa Rais amesema ni muhimu kwa Mkutano huo kujadili
hatua za haraka za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na athari zake
ikiwa ni pamoja na mbinu jumuishi zinazolenga kulinda maisha ya jamii na
kuimarisha ulinzi wa mazingira dhidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi.
Amesema mabadiliko ya tabianchi kwa upande mwingine yana fursa nyingi
katika kutengeneza ajira Barani Afrika ikiwemo katika mchakato wa
kupunguza athari, kuna ajira ambazo zinatengenezwa hususani pale wakulima
wanapotumia kilimo hai na utafutaji na ukuzaji wa mbegu na malisho kwa
jamii za wafugaji. Vile vile, amesema katika mapinduzi ya kijani kuna fursa za
ajira zilizoundwa kwa kuweka kipaumbele kwa nishati safi hususani nishati
jua, jotoardhi, upepo na maji.
Makamu wa Rais amesema Tanzania imedhamiria kutengeneza ajira milioni 7
kati ya mwaka 2020-2025 ambapo mikakati ya utekelezaji wa lengo hilo ni
pamoja na kuboresha mazingira ya biashara, uanzishwaji wa kanda maalum
za kiuchumi katika halmashauri zote za wilaya nchini zenye miundombinu
inayohitajika kwa ajili ya wanawake, vijana na watu wenye mahitaji maalum ili
kufanya shughuli za uzalishaji mali. Amesema mikakati mingine ni pamoja na
kutoa mafunzo na kuwaunganisha vijana na taasisi zinazotoa mikopo nafuu
ikiwemo kuanzisha programu ya Jenga Kesho Bora: Mpango wa Vijana kwa
Biashara ya Kilimo (BBT-YIA) na ile ya Sekta ya Mifugo (BBT-Live) kwa ajili ya
uzalishaji wa nyama ya ng'ombe na ufugaji wa Samaki. Pia uanzisha vituo
vilivyotengwa ambapo vijana wataweza kujifunza na kupata ujuzi wa vitendo
utakaowawezesha kujihusisha na uzalishaji pamoja na kutenga asilimia 10 ya
mapato ya kila halmashauri ya wilaya kwa ajili ya wanawake, vijana na watu
wenye mahitaji maalum.
Mkutano huo unafanyika tarehe 7-8 Februari 2024 umeandaliwa na Chama
cha Waajiri Tanzania (ATE) kwa Kushirikiana na Shirika la Kimataifa la Waajiri
(IOE).
Imetolewa na
Ofisi ya Makamu wa Rais
07 Februari 2024
Dar es salaam.

