Wananchi wa Halmashauri ya Mpimbwe wilayani Mlele wameondokana na adha ya kutumia mikokoteni ya ng'ombe na baiskeli kubeba wagonjwa kwenda vituo vya afya kupata matibabu baada ya kupata magari mawili.
Magari hayo yametolewa na serikali kupitia wizara ya afya ili kunusuru maisha ya wagonjwa, wajawazito na watoto hususani wakati wa kujifungua.
Wakizungumza leo Jumatano February 7,2024 baadhi ya wananchi wamesema wagonjwa walipoteza maisha kwa kushindwa kufikishwa vituo vya afya kwa wakati.
Jaklina Kapamya mkazi wa Usevya amesema kabla ya kupata magari hayo iliwalazimu kukodi gari kupeleka mgonjwa au kutumia baiskeli na mikokoteni .
"Ukiwa hauna uwezo wa kukodi gari mgonjwa anapoteza maisha hivyo tunashukru sana serikali kutupatia magari haya mawili,"amesema Jakline.
Leopord Mbogo mkazi wa Usevya amesema akinamama hususani wajawazito wakati wa kujifungua uhai wao utapatikana kwasasa.
"Walikuwa wanapoteza maisha kwasababu ya kukosa usafiri wa haraka gari lililokuwepo ni moja halikidhi mahitaji,"amesema Mbogo.
Mganga Mfawidhi wa kituo cha afya Usevya Seni Ngusa amesema wamekuwa na changamoto kubwa ya kusafirisha wagonjwa wa dharura.
"Tulikuwa na gari moja la kubebea wagonjwa pia hatukuwa na gari la usimamizi ujio wa magari haya itasaidia sana,"amesema Ngusa.
"Kiutendaji ilituathiri wakipatikana wagonjwa mahututi wakiwa sehemu mbili tofauti ilibidi gari liende Mpanda likirudi ndiyo lichukue mwingine,"
Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya Mpimbwe Shamim Mwariko amesema hadi sasa kuna vituo 17 vya kutolea huduma za afya.
'Pia tuna hospitali moja, vituo vya afya sita na zahanati kumi lakini gari la kubebea wagonjwa lilikuwa moja,"amesema Mwariko.
Ameongeza kuwa ujio wa magari hayo mawili itasaidia kutatua changamoto ya usafiri kurahisisha huduma za dharura.
Mwisho.
