Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amesema Serikali imeamua
kwa dhati kuendeleza vyanzo vya umeme wa Jotoardhi ili kuhakikisha nchi inazalisha umeme
wa kutosheleza mahitaji ya wananchi wake.
Amesema chanzo hicho cha umeme kitaongeza nguvu katika vyanzo vilivyopo vya Maji na Gesi
Asilia.
Dkt. Biteko amesema hayo tarehe 20 Februari, 2024 wilayani Rungwe, Mkoa wa Mbeya mara
baada ya kukagua vyanzo vya Jotoardhi vya Kiejo-Mbaka (60MW) na Ngozi (MW 70) mkoani
humo akifuatana na viongozi mbalimbali wa Mkoa wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa, Juma
Homera.
" Miradi hii ya Jotoardhi sasa lazima ianze, tutaanza na megawati 10 hapa Kiejo-Mbaka na
Ngozi tutaanza na megawati 30 huku nyingine zikifuata, na hii inajumuisha miradi mingine
kama wa Jua wa Kishapu (150 MW) ambao umeanza kutekelezwa, miradi ya umeme wa upepo
ukiwemo wa Makambako na mradi wa Malagarasi ambao mkandarasi ameshasaini mkataba
tayari kwa kuanza kazi." Amesema Dkt. Biteko
Amewaelekeza watendaji wa Kampuni ya Uendelezaji wa Jotoardhi Tanzania (TGDC) kufanya
kazi zinazoleta matokeo na si stori kwani Serikali inatafuta fedha za kutekeleza miradi hiyo na
wajibu wa watendaji wa Taasisi hiyo ni kuhakikisha miradi hiyo inafanikiwa.
Dkt. Biteko amesema kuwa, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu
Hassan anataka kuona watanzania wanapata huduma bora katika sekta zote, wanatolewa
kwenye umaskini, anataka vitendo na siyo maneno, anataka kuona watu wahudumiwa na
kufuatwa walipo, wanasikilizwa shida zao na kutatuliwa.
Ameongeza kuwa, Rais, Dkt. Samia anataka utekelezaji wa mipango mbalimbali ya Serikali
iangalie miaka mingi mbele na si muda mfupi hivyo ametoa uhakika kwa wananchi kuwa miradi
hiyo ya Jotoardhi itatekelezwa.
Kuhusu changamoto ya umeme, amesema kuwa, imetokana na vyanzo vya umeme nchini kwa
muda mrefu kujikita kwenye makundi matatu tu ambayo ni maji (570MW), Mafuta na Gesi
Asilia.
Amesema kwa sasa, vyanzo vya umeme vinatokana na Gesi Asilia na Maji ambavyo bado
havitoshelezi mahitaji kutokana na kuzidi kukua kwa maendeleo, idadi ya watu kuzidi
kuongezeka, miji kukua na umeme sasa kuwa ni hitaji muhimu na si anasa.
Amesema pamoja na kutegemea megawati 235 kutoka mradi wa Julius Nyerere (JNHPP) na
megawati 27 kutoka Rusumo, maboresho ya mitambo mingine ya umeme yanaendelea katika
vituo mbalimbali.
Aidha, ameeleza kuwa, Serikali imeshaamua kutekeleza vyanzo vingine vya umeme ikiwemo
vya Jotoardhi, Jua na Upepo kwani vipo na kinachohitajika ni kuvipa nguvu,
Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko amepongeza viongozi wa Mkoa wa Mbeya kwa usimamizi
mzuri wa miradi ya maendeleo pamoja na ushirikiano uliopo kati ya viongozi wa Serikali na
Wabunge wa Mkoa huo.
Awali, Meneja Mkuu wa TGDC, Mhandisi Mathew Mwangomba, amesema kampuni hiyo ina
miradi mitano ya kipaumbele nchini ambayo ni Kiejo-Mbaka, Ngozi, Songwe, Ruhoi na Natron.
Ameeleza kuwa, kwa Mkoa wa Mbeya miradi ya kipaumbele ni Ngozi na Kiejo-Mbaka ambapo
mradi wa Ngozi unatarajiwa kuzalisha megawati 70 na Kiejo-Mbaka unatarajiwa kuzalisha
megawati 60.
Katika mradi wa Ngozi, amesema kuwa, utatekelezwa kwa awamu huku awamu ya kwanza
ikitarajiwa kuzalisha megawati 30 na fedha zimeshapatikana ili kuhakiki rasilimali ya Jotoardhi
kwenye eneo hilo.
Ameongeza kuwa, mradi huo wa awali utakaozalisha megawati 30 utagharimu Dola za
Marekani milioni 144 sawa na shilingi bilioni 369.
Kuhusu mradi wa Kiejo-Mbaka, amesema kuwa, unatarajiwa kuzalisha megawati 60 ambapo
zitaanza kuzalishwa megawati kumi (10) ambazo utekelezaji wake utagharimu Dola za Marekani
milioni 75.64 sawa na shilingi Bilioni 175.88.
Ameongeza kuwa, katika kuhakikisha nishati ya Jotoardhi inapatikana Tanzania, TGDC
imechonga visima vifupi vya mita 300 ambavyo viliwezesha kupatikana kwa temperature
takriban 75 na hii ikithibitisha kwamba kuendelea kuchimbwa kwa visima hivyo kuanzia mita
1500 hadi 1900 itapatikana temperature ya kutosha kuweza kuzalisha umeme.
Vilevile amesema kuwa, nishati ya Jotoardhi ina umuhimu mkubwa nchini kwani ni hakika,
endelevu na salama hasa katika kipindi hiki ambacho dunia inapambana na mabadiliko ya tabia
nchi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera amemhakikishia Naibu Waziri
Mkuu na Waziri wa Nishati kuwa, Mbeya inamuunga mkono Rais, Dkt. Samia katika kulinda
vyanzo vyote ya umeme vinavyogundulika pamoja na utunzaji wa mazingira ambayo
yanapelekea vyanzo hivyo kuzalisha umeme kwa ufanisi.
Pia amempongeza Dkt. Biteko kwa ubunifu wake katika kuendeleza vyanzo vipya vya umeme
ukiwemo wa Jotoardhi.
Caps
moja
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt.Doto Biteko akishuhudia kufunguliwa kwa
valvu ya kuruhusu majimoto yanayotoka ardhini kupita katika kisima cha utafiti wa Jotoardhi
katika eneo la Kiejo-Mbaka wilayani Rungwe mkoani Mbeya. Anayefungua valvu ni Meneja
Mkuu wa Kampuni ya Uendelezaji wa Jotoardhi Tanzania ( TGDC), Mhandisi Mathew
Mwangomba.
mbili
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko akipanda mti katika eneo
lenyo chanzo cha Jotoardhi, Kiejo-Mbaka wilayani Rungwe mkoani Mbeya ikiwa ni ishara ya
utunzaji wa mazingira ambayo ni muhimu katika uzalishaji wa nishati ya umeme nchini
