Taasisi za umma zinazolisha watu zaidi ya 100 kwa siku kutoka katika Wizara
sita zimetekeleza maelekezo ya Serikali ya kuhama kutoka matumizi ya kuni
na mkaa na kuhamia katika matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imekuwa kinara kwa taasisi zake
kutekeleza agizo hili la Serikali kwa zaidi ya asilimia 85.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano
na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo wakati akizungumza na waandishi wa
habari leo Februari 20, 2024 Jijini Dodoma wakati akitoa taarifa ya utekelezaji
wa maelekezo ya usitishaji wamatumizi ya kuni na mkaa kwa taasisi za
umma.
Amesema lengo la maelekezo hayo ni kupunguza madhara ya kiafya na
mazingira yanayosababishwa na kukithiri kwa matumizi ya kuni na mkaa
katika jamii zetu na ukataji wa miti kwa ajili ya nishati ya kupikia.
Dkt. Jafo amesisitiza kuwa katazo hilo haliwahusu watumiaji katika ngazi ya
kaya na watumiaji wadogo bali limeanza kwa watumiaji wakubwa na Serikali
inaendelea kutoa elimu kwa wananchi hao ili waanze kutumia nishati safi ya
kupikia
“Kama nilivyosema awali Taasisi hizo ziko chini ya Ofisi ya Rais Tawala za
Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga
Taifa, Wizara ya Afya, Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Makundi
Maalum, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia pamoja na Wizara ya
Mambo ya Ndani ya Nchi,” amesema Dkt. Jafo.
Dkt. Jafo amesema Sera ya Taifa ya Mazingira ya mwaka 2021 inahimiza
umuhimu wa kulinda na kuhifadhi mazingira ikiwemo rasilimali za misitu, hivyo
ili kufikia lengo hilo, Sera inahamasisha matumizi ya nishati mbadala wa kuni
na mkaa kwa lengo la kupunguza ukataji miti na uharibifu wa misitu.
Ameongeza kuwa Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais ilitoa katazo la
matumizi ya kuni na mkaa kwa taasisi zinazoandaa na kulisha watu zaidi ya
mia moja (100) kwa siku, ifikapo Januari, 2024 ambapo katika taarifa yake ya
utekelezaji Wizara hizo zimetuma mipango husika ya matumizi ya nishati
mbadala na jinsi zitakavyotekeleza agizo hili.
Kwa mujibu wa Dkt. Jafo, katika sekta ya Elimu hadi kufikia Januari 31,
mwaka huu jumla ya Vyuo vya Ualimu 30 kati ya 35 sawa na asilimia 85.71 ya
lengo, Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi 51 kati ya 54 sawa na asilimia
94.44 ya lengo, na Vyuo vya Elimu ya Ufundi (VETA) vinane (8) kati ya 36
sawa na asilimia 22.22 vimeshaunganishwa na huduma ya Nishati Mbadala
ya Kuni Poa.
Amefafanua kuwa Sekta ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na
Makundi Maalum, kuna jumla ya Taasisi 8 ambapo 6 ni vyuo vya maendeleo
ya Jamii na taasisi mbili ni vyuo vya maendeleo ya jamii na ufundi. Vyuo vya
Maendeleo ya Jamii Tengeru na Uyole kwa sasa vimeanza kutumia Nishati
mbadala sawa na asilimia 25 ya lengo.
Aidha Dkt. Jafo ameeleza kuwa katika Sekta ya Afya hadi kufikia Januari 31
mwaka huu Hospitali tatu (3) ikiwemo Hospitali ya Rufaa ya Mkoa
Mwananyamala (DSM), Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Dodoma na Kituo cha
Afya Sinza (DSM) tayari zimeanza kuzalisha gesi.
Kuhusu taasisi zilizopo Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Chuo cha Chuo
cha Maafisa wa Polisi Kidatu na shule ya Polisi Tanzania zinatumia majiko
yenye mfumo wa gesi. Na baadhi ya vyuo ikiwemo Chuo cha Polisi Zanzibar
wanatumia gesi na kuni kidogo.
“Jeshi la Magereza lina jumla ya Magereza 129, Vyuo vya Magereza vinne (4)
na Shule za Sekondari Bwawani. Kati ya vituo hivyo jumla ya Magereza 76
sawa na asilimia 58.91, Vyuo 3 sawa na asilimia 75 ya vyuo vya magereza,
na Sekondari ya Bwawani yameanza kuacha kutumia kuni na mkaa na
kuanza kutumia nishati mbadala ikiwemo gesi asilia” amesema Dkt. Jafo.
Katika Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Jafo amesema asilimia
90 ya baadhi ya vikosi vinatumia nishati mbadala kama vile gesi wakati huo
vikosi vingine vikiwa vimetekeleza kwa kiwango cha wastani kwa kupunguza
matumizi ya kuni na mkaa na kuanza kutumia gesi.
Aidha Dkt. Jafo amesema katika Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Mamlaka
za Serikali za Mitaa (TAMISEMI), ambayo inamiliki kiwango kikubwa cha
shule za Msingi na Sekondari nchini, jumla ya shule 571 za bweni zenye
wanafunzi wapatao 156,622. Kati ya shule hizo za bweni, shule 67 sawa na
asilimia 11.73 zimefungwa mifumo ya gesi ambapo shule 60 kati ya hizo
zinatumia mufumo ya gesi.
Amesema kuwa Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kushirikiana na Wizara za
Kisekta ipo kwenye maandalizi ya kuunda Timu ya Wataalam itakayoweza
kutembelea taasisi husika ili kufuatilia hatua zinazoendelea katika utekelezaji
wa katazo hilo na kutoa ushauri wa kitaalam.
Itakumbukwa kuwa tarehe 01 Novemba, 2022, Jijini Dar es Salaam, Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan
alizindua Mjadala wa Kitaifa wa Nishati Safi ya Kupikia ambapo aliekeza
kusitisha matumizi ya kuni na mkaa kwa taasisi zinazolisha watu Zaidi 100
kwa siku, ifikapo Januari 31, 2024.