Waziri wa Afya Mhe.Ummy Mwalimu ametoa wito kwa wazazi wenye Watoto wenye tatizo la Selimundu(Sickle Cell) kupeleka kwa watalaam wa Afya kuambatana na watoto wasio kuwa na tatizo hilo ili kupata ushauri wa kitaalam ikiwemo kupandikizwa uloto .
Mhe.Ummy amesema hayo Jijini Dodoma katika Uzinduzi wa Huduma za Upandikizaji Uloto Hospitali ya Benjamin Mkapa uliokwenda sambamba na kauli mbiu isemayo” Ugonjwa wa Selimundu(Sickle Cell) unatibika na kuondoshwa kabisa”.
Waziri Ummy wakati akitoa elimu kwa kumtambulisha mtoto Ester Osena aliyemsaidia kaka yake Elisha Osena kwa kupandikizwa Uloto amesema ni muhimu wazazi wenye watoto wenye tatizo la Selimundu kuambatana na watoto wao wengine wasio kuwa na tatizo hilo ili kuweza kuokoa Maisha yaw engine.
“Nataka kutoa wito kwa wazazi kama una mtoto mwenye Sickle Cell na una watoto wengine wazima ,Ester huyu leo ni shujaa ,Ester ana miaka 6 ,amemchangia Uloto kaka yake anaitwa Elisha ,amempa uhai ,kwa sababu watoto wengi wenye matatizo ya Sickle Cell wanafariki dunia kabla ya kufikisha miaka mitano, lakini nampongeza baba na mama Ester kwa kuwaamini wataalam wetu kwa sababu ametolewa kitu mwingine anasema binti yangu mzuri huyu mnakwenda kumchokonoachokonoa nitampoteza lakini Ester amemrejeshea furaha kaka yake Elisha tunamwona Ester mzima hana tatizo ,wataalam wanasema kabla ya miaka 12 mtoto anaweza kupandikizwa Uloto, nimetumia muda huu kuelimisha wazazi leteni watoto mkiambatana na watoto wazima wa damu ili kuokoa ndugu zao”amesisitiza Mhe.Ummy.
Aidha, Waziri Ummy amesema kila mwaka takriban watoto 11,000 huzaliwa na tatizo la Selimundu hapa nchini ambapo kwa mwaka huu serikali ina mpango wa kudhamini watoto 20 kupandikizwa uroto bure huku akiweka msisitizo kwa viongozi ngazi zote kuwajibika.
“Mwaka huu tutadhamini watoto 20 kupandikizwa Uloto bure ,wajibu wetu sisi Viongozi wakiwemo wa Wilaya ,Wizara ni kuhakikisha tunasimamia huduma bora za afya zinatolewa”.
Hali kadhalika Waziri Ummy amesema kuna mpango wa kupandisha hadhi Hospitali ya Benjamin Mkapa na kuwa Hospitali ya Taifa kwendana na hadhi ya makao makuu ya nchi Dodoma.
