Makamu Wakuu wa Vyuo, Manaibu Makamu Wakuu wa Vyuo na Marasi leo Mei 11, 2023 wanapitia rasimu ya Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 toleo la 2023 na rasimu ya mitaala ya Elimu ya Awali, Msingi, Sekondari na Ualimu.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao kazi hicho Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Carolyne Nombo amesema lengo ni kuendelea kuwapa nafasi Wakuu wa Vyuo kutoa maoni kwenye rasimu hizo.
"Sote tunafahamu mitaala ni chombo cha utekelezaji wa Sera hivyo Sera nayo imefanyiwa mapitio ili itoe miongozo ya utekelezaji," amesema Prof. Nombo
Amesema kupitia Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET) Vyuo Vikuu navyo vinafanya mapitio ya mitaala hivyo kushiriki kutoa maoni katika rasimu ya Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 toleo la 2023 na mitaala ya Elimu ya Awali, Msingi, Sekondari na Ualimu kutasaidia katika hatua ya kufanya maboresho kwenye mitaala ya vyuo vikuu.
"Kupitia Mradi wa HEET mtafanya mapitio ya mitaala kwa hiyo ni muhimu kuona mapendekezo yaliyowekwa kwenye rasimu hizi ili mjue mnapohuisha mitaala ya elimu ya juu wanaokuja walivyoandaliwa," amesema Prof. Nombo.
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Prof. James Mdoe amesema kufanyika kwa mapitio ya Sera ya Elimu na Mafunzo kwa mwaka 2014 na mabadiliko ya Mitaala ni maelekezo ya Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili kuhakikisha elimu tunayotoa inajenga umahiri na ujuzi.

