WAKAZI WA RUFIJI MKOANI PWANI WAIPONGEZA WIZARA YA MALIASILI NA UTALII KWA KUTOA MAFUNZO YA MAZAO YA MISITU.

MUUNGANO   MEDIA
0

Wakazi wa Halmashauri ya Rufiji Mkoani Pwani wameipongeza Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kutoa mafunzo ya mazao ya misitu huku wakiahidi kuwa elimu waliyoipata itatumika kuwanufaisha Wananchi wote wa Mkoa wa Pwani katika kulinda Maliasili za nchi pamoja na kufuga nyuki kibiashara.

Akizungumza leo wilayani Rufiji kiongozi wa ziara ya Mafunzo ya Utekelezaji wa Sera ya Misitu na Sera ya Ufugaji Nyuki kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii,  Emmanuel Msoffe  amesema mafunzo hayo  ni muhimu kwa wakazi wa Rufiji ambapo yatakwenda kuwasaidia kujua namna bora ya  kuhifadhi na kutunza  misitu kwa faida ya kizazi cha sasa na cha baadae.

 Amesema Wizara ya Maliasili na Utalii imeamua kutoa  mafunzo hayo kwa Wana Rufiji  ili kuwapa  uelewa mkubwa ambao utawasaidia  wakazi hao juu ya namna bora ya kuifanya misitu kuwa endelevu.

Msoffe amesema mara baada ya mafunzo  hayo Wadau  wamewaelezea  changamoto na mafanikio mbalimbali  wanayoyapata katika shughuli za uhifadhi   lakini hata hivyo Wadau  hao wamekiri kuwa  wamépata uelewa mkubwa kupitia mafunzo hao ambayo yatawasaidia kubadilishana mawazo na uzoefu ambao watautumia  katika kutekeleza shughuli za Misitu na Nyuki.

Aidha, amesema mbali na kuelezwa changamoto zinazowakabili wakazi wa eneo hilo ikiwemo ya wafugaji kuingiza mifugo kwenye mashamba yao pamoja na uvunaji haramu wa mazao ya misitu, ziara imekuwa na mafanikio makubwa .

Kwa upande wake   Mdau wa Misitu kutoka wilaya ya Rufiji, Mohammed Salum ameipongeza Wizara kwa  kufanya kazi kubwa ya kutoa elimu  ya  mazao ya misitu kwani itawasaidia kupata kipato cha mtu mmoja mmoja na kuleta maendeleo kwa taifa kwa ujumla.

"" Faida tunaijua na tumeiona, elimu mnayotupa mara kwa mara  kuhusiana na  uhifadhi wa misitu na ufugaji nyuki inatusaidia sana kuwa mabalozi wazuri wa uhifadhi hapa nchini " amesema Mohammed.

Ameongeza kuwa elimu ya kulinda misitu na kufuga nyuki ambayo wamekuwa wakipewa mara kwa mara imekuwa msaada mkubwa  kwani kwa sasa mazao ya misitu yamekuwa yakiwaingizia  kipato kilichowawezesha kujenga ofisi ya kijiji, shule,  wodi ya kina mama pamoja na maabara.

Tags

Chapisha Maoni

0Maoni
Chapisha Maoni (0)