Na Angela Msimbira, MOROGORO.
Ofisa Elimu Mkoa wa Morogoro Bi. Germana Mung 'aho amewataka Wahandisi na Maafisa Manunuzi nchini kuhakikisha wanasimamia miradi ya maendeleo kwa weledi na kwa kuzingatia ubora wa majengo.
Mung’aho ameyasema hayo leo Mei 3, 2023 alipokuwa akifungua Mafunzo ya Siku mbili kwa Wahandisi na Maafisa Manunuzi wa Halmashauri yanayofanyika mkoani Morogoro kuhusu ujenzi wa miundombinu ya shule za elimu ya awali na msingi zinazojengwa kupitia mradi wa Boost.
“Kuna kila sababu ya ya kuhakikisha tunasimamia miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika Halmashauri zetu kwa weledi ili thamani ya miradi iweze kuonekana," amesema Bi. Mung'aho.
Amesema serikali imejikita katika kuhakikisha miradi inayotekelezwa katika Mamlaka za Seriakali za Mitaa inakamilika kwa wakati nchini."Tunaposema mradi utakamilika ndani ya miezi mitatu tunataka nchi nzima iwe imekamilika kwa wakati hivyo kila Mkoa unawajibu wa kuhakikisha inakamilika hatutaki Mkoa mmoja unakamilisha mwingine bado,” amesema.
Aidha, amewataka Maafisa hao kuhakikisha wanashirikiana na idara nyingine katika utekelezaji wa miradi ili kuleta matokeo chanya.
“Wahandisi angalieni ramani hakikisheni mnasimamia kila hatua ya ujenzi na nyie Maafisa Ununuzi hakikisheni mnaweka uzalendo katika kufanya manunuzi angalieni unafuu wa gharama na ubora wa vifaa vinavyohitajika kwenye miradi ya maendeleo ili kuipunguzia gharama serikali,”amesema.
Naye Mratibu wa Mafunzo kituo cha Morogoro kutoka Ofisi ya Rais -TAMISEMI Bw.Yusuph Singo amesema lengo la mafunzo kuwajengea uelewa wa pamoja kuhusu ramani na michoro itakayotumika katika ujenzi na kuelekezwa taratibu za manunuzi.
Aidha, amesema mafunzo hayo yatawasaidia kujua utaratibu wa ujenzi kupitia mradi wa Boost na suala la usalama wa mazingira na jamii.


