Uturuki yajijitolea kuandaa mazungumzo ya upatanishi wa mgogoro wa Sudan, Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki ametangaza jana kuwa nchi yake iko "tayari kuandaa mazungumzo" kwa lengo la kutatua mgogoro wa sasa huko Sudan ikiwa uamuzi utachukuliwa na pande zinazozozana kuanzisha mazungumzo ya kina.
Katika mazungumzo ya simu na mwenyekiti wa Baraza Kuu la Utawala Sudan, Jenerali Abdel Fattah al-Burhan ambaye pia ni mkuu wa jeshi la nchi hiyo, Erdogan "ameelezea huzuni na wasiwasi wake" juu ya kuongezeka kwa idadi ya wahasiriwa katika mzozo wa kijeshi uliozuka katikati ya Aprili, taarifa kutoka Kurugenzi ya Mawasiliano ya Türkiye imesema.
Wakati mazungumzo ya kusitisha mapigano kati ya pande hasimu za Sudan yalianza Jumamosi katika mji wa pwani wa Saudi Arabia wa Jeddah, yakiungwa mkono na Marekani, mwanadiplomasia wa Saudia aliiambia AFP siku ya Jumatatu kwamba mazungumzo hayo hayajazaa matunda kwani "hakuna hatua kubwa zilizochukuliwa."
Mapigano makali, ambayo yalizuka kutokana na mzozo wa madaraka kati ya Jeshi la Sudan (SAF) linaloongozwa na Jenerali Abdel Fattah al-Burhan na Kikosi cha Radiamali ya Harakati (RSF) kinachoongozwa na Mohamed Hamdan Dagalo ambaye ni maarufu kama Hemetti yamesababisha vifo vya takriban watu 550, na karibu 5,000 kujeruhiwa tangu Aprili 15.
Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi linatafuta dola milioni 445 kwa ajili ya kutoa msaada wa haraka kwa takriban wakimbizi 860,000 nchini Sudan.
Erdogan, ambaye anawania muhula wa tatu kama rais katika uchaguzi wa Mei 14, anajaribu kuidhihirisha Uturuki kama mpatanishi katika migogoro mingine, ikiwa ni pamoja na mgogoro wa Russia na Ukraine.
Chanzo #Parstoday.