TARURA MOROGORO YASHAURIWA KUSIMAMIA MIRADI..

MUUNGANO   MEDIA
0

Kamati ya Ukaguzi ya Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), imeishauri Ofisi ya TARURA Mkoa wa Morogoro kusimamia miradi kwa ukaribu na ufanisi wa hali ya juu ili miradi iweze kukamilika kwa wakati na ubora.

Hayo yameshauriwa na Wajumbe wa Kamati inayongozwa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Ndugu CPA. Ally Rashid Ally, Mkaguzi Mkuu wa Ndani (CIA), wa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR - TAMISEMI), walipokuwa katika ziara ya ukaguzi wa miradi katika Mkoa huo.

“Jukumu kubwa la kamati hii ni kushauri nini kifanyike ili tuweze kuleta tija katika miradi yetu na wananchi waweze kunufaika na miradi hii ikiwa kwenye ubora ule unaotakiwa pale ambapo itakamalika kwa wakati’’, alisema Ndugu Ally.

Aidha, pamoja na usimamizi wa karibu katika miradi hiyo kamati imeishauri Ofisi ya TARURA Mkoa wa Morogoro itoe mikataba kwa kuzingatia vipindi vya mvua, usimamizi wa mikataba kwa weledi, uwekaji wa alama za barabarani pamoja na uwekaji wa vivuko kwenye mitaro.

Kwa upande wake Meneja wa TARURA Mkoa wa Morogoro, Mhandisi Emmanuel Ndyamukama amesema kuwa wataendelea kusimamia miradi hiyo kwa ukaribu pamoja na kuyafanyia kazi yale yote yaliyoshauriwa na kamati ili wananchi waweze kunufaika na miradi.

Aidha, ameongeza kuwa TARURA Mkoa wa Morogoro watahakikisha wanafanyia kazi maeneo yote yaliyobainishwa yenye mapungufu kwenye miradi iliyokaguliwa ili kuleta tija na kuonesha thamani ya fedha katika miradi ambayo kamati imetembelea.

“Kamati imetushauri mambo mengi katika usimamizi wa karibu wa miradi ushauri wote tumeupokea na tutafanyia kazi kama ambavyo kamati imetushauri ili kuondoa yale yote yanayoweza kuepukika’’ alisema.

Kamati ya Ukaguzi ya TARURA imeanza ziara yake mkoani Morogoro katika ujenzi wa Daraja la Berege lenye urefu wa mita 140 ambapo ujenzi wake umefikia asilimia 73, ujenzi wa daraja la Ruhembe lenye urefu wa mita 40 ambapo ujenzi wake umefikia asilimia 43 pamoja na ujenzi wa barabara ya Wami-Dakawa – Kibaoni kwa kiwango cha lami yenye urefu wa Km 0.80, Kamati itaendelea na ziara yake katika Mkoa wa Tanga na Kilimanjaro.

Tags

Chapisha Maoni

0Maoni
Chapisha Maoni (0)