Timu ya mpira wa pete ya ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa ( OR-TAMISEMI) TAMISEMI Queens imeagwa rasmi 12 Mei 2023 kuelekea nchini Kenya ambako itashiriki katika mashindano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki mchezo wa hup yatakayoanza rasmi 13 hadi 20 Mei 2023.
Akizungumza wakati wa kuagana na timu hiyo Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia Afya Ofisi ya Rais -TAMISEMI, Dkt. Charles Mahera ameitaka timu hiyo kushiriki kikamilifu katika michuano hiyo na kuhakikisha inaibuka kidedea katika michuano hiyo.
"Mnakwenda kwenye mashindano haya na nimeambiwa sio mara yenu ya kwanza kushiriki mwaka jana mlishika nafasi ya nne mwaka huu mkajitahidi kushika nafasi ya kwanza" Amesema Mahera
Mahera amesisitiza kuwa Ofisi ya Rais-TAMISEMI itaendelea kuiongezea nguvu timu hiyo kwakuwa michezo ni sehemu ya malengo ya kitaifa ya kuhakikisha jamii inandokana na magonjwa mbalimbali hususan magonjwa yasio ya kuambukiza.
Kwa upande wake Kempteni wa timu hiyo Bi. Dafroza Luhwgo ameihakikishia Ofisi ya Rais-TAMISEMI kuwa timu hiyo imejifua vilivyo na itahakikisha inaipeperusha vyema bendera ya Tanzania kwa kuibuka kidedea katika michuano hiyo.

