Baadhi ya Watumishi wakiwamo Madiwani wa halmashauri ya Mlele Kati yao wameshikilia tuzo walizozawadiwa.Picha na Mary Baiskeli.
Na Mary Baiskeli, Katavi.
Halmashauri ya wilaya ya Mlele imeanzisha utaratibu wa kuwatunuku tuzo watumishi bora ili kuwaongezea morali ya kufanya kazi kwa weledi ikiwa ni pamoja na kuwaepusha na tabia ya kuomba uhamisho pasipo sababu za msingi.
Utaratibu huo umeanza katika kikao cha baraza la Madiwani wa halmashauri hiyo baada ya kuwatunuku tuzo za heshima watumishi 21 walioonesha kufanya uzalendo katika utendaji kazi wao.
Awali Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo Teresia Irafay amesema wamefikia uamuzi huo lengo ni kuwatia moyo watumishi hao wachache badala ya wengi ili walete changamoto ya kuongeza bidii kiutendaji na kusukuma gurudumu la maendeleo.
“Kama menejimenti tuliona tuwape zawadi wale waliopongezwa na Mkuu wa mkoa Mwanamvua Mrindoko tarehe mosi Mei,2023 katika sikukuu ya wafanyakazi,”
“Kwakushirikiana na baraza tutatoa zawadi hizi pia kwa viongozi wengine wakiwamo Madiwani kwa kutambua umhimu wao wa kuleta maendeleo katika halmashauri ya Mlele,” amesema Irafay.
Kwaupande wake Mkuu wa wilaya ya Mlele Majid Mwanga amepongeza hatua hiyo akidai kuwa kufanya hivyo ni motisha tosha kwa watumishi hao.
“Nilisikia mijadala watumishi wanahama nikaogopa kidogo lakini kwa hili nawapongeza, wakati mwingine mtumishi haihitaji hata shilingi yako anahitaji pongezi ya maneno pekee,”
“Hongereeni sana wanajisikia vizuri naomba Waheshimiwa Madiwani wajengeeni nyumba watumishi nzuri ili waishi maisha mazuri,”amesema Mwanga.
Sanjari na hayo katika kikao hicho cha baraza la Madiwani kilichoketi kwaajili ya kusomewa taarifa za maendeleo ya kamati kimeridhia kwa pamoja kuwapandisha vyeo watumishi 21.
Mwenyekiti wa halmashauri hiyo Soud Mbogo akizungumza kwa niaba ya Madiwani hao baada ya kujigeuza kuwa kamati na kupitia mapendekezo ya kiutumishi wamekubaliana kuwapandisha vyeo watumishi wasio walimu.
“Baraza kwa kauli moja limeridhia watumishi hao wapandishwe vyeo kama mapendekezo yalivyowasilishwa ambapo baraza limeacha jukumu kwa Mkurugenzi kuendelea na hatua inayofuata,”amesema Mbogo.
Hata hivyo imeelezwa kuwa watumishi wengi wa halmashauri ya Mlele wamekuwa wakiomba uhamisho jambo ambalo limezua sintofahamu.
