Watumishi watatu waliochaguliwa kuwa wafanyakazi bora wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa mwaka 2023 wamekiri kuwa, kitendo cha Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kujali na kusimamia stahiki na maslahi ya watumishi wa umma nchini kimewamotisha kufanya kazi kwa bidii na hatimaye kuchaguliwa kuwa wafanyakazi bora wa ofisi hiyo.
Mmoja wa watumishi hao ambaye ni Afisa Utumishi Bi. Frida Byakuzana aliyeshika nafasi ya tatu amesema, ufanyakazi bora alioupata umechagizwa na kitendo cha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kujali maslahi ya watumishi wa umma kwa kuwapandisha madaraja, kulipa madai ya malimbikizo ya mishahara, kuboresha posho ya kufanya kazi katika muda wa ziada pamoja na posho ya safari za ndani ya nchi.
“Kitendo cha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kuboresha maslahi ya Watumishi wa Umma nchini kimekuwa ni chachu kwangu ya kufanya kazi kwa bidii na weledi ili kuweza kufikia lengo la Serikali ya Awamu ya Sita la kutoa huduma bora kwa wananchi,” Bi. Byakuzana amefafanua.
Bi. Byakuzana ametoa wito kwa watumishi wa umma kuendelea kufanya kazi kwa bidii na ubunifu ikiwa ni sehemu ya kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye tangu aingie madarakani amekuwa mstari wa mbele kusimamia maslahi ya watumishi wa umma kwa lengo la kujenga ari na morali ya watumishi wa umma katika kutoa huduma bora kwa wananchi pamoja na kutoa mchango katika maendeleo ya taifa.
Kwa upande wake, Afisa Utumishi Bw. Juma Senzota aliyeshika nafasi ya pili ameahidi kuendelea kutoa huduma bora kwa watumishi wa umma wanaofuata huduma katika Ofisi ya Rais-UTUMISHI akiamini kuwa kitendo hicho kitawajengea morali watumishi hao kwenda kutoa huduma bora kwa wananchi katika maeneo yao ya kazi na hatimaye kutimiza azma ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuboresha huduma kwa wananchi pamoja na kuliletea taifa maendeleo