UZINDUZI WA TAMASHA LA ZIFIUKUKI WAFANA

MUUNGANO   MEDIA
0
TAZAMA VIDEO HAPA CHINI


Na WMJJWM, Dar es salaam


Serikali imezindua rasmi Tamasha la kuonesha fursa za Maendeleo na kupinga ukatili lenye kaulimbiu ya Zijue Fursa, Imarisha Uchumi, Kataa Ukatili, Kazi Iendelee (ZIFIUKUKI) Leo tarehe 28 Aprili, 2023.


Akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dorothy Gwajima, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. John Jingu ametoa wito kwa wadau wote kupambana na mmomonyoko wa maadili ndani ya jamii kwani vitendo vyote vya ukatili vinatokana na kukosa maadili mema.


Dkt. Jingu amesema mabalozi wote waliotangaza kutokomeza ukatili wakiwemo wasanii, viongozi wa dini, wazazi, walezi, wanasiasa, wanamichezo, walimu na wazee ni nyenzo muhimu kwani wana ushawishi mkubwa kwenye jamii.


"Wasanii tumieni ushawishi mlionao kupambana, matarajio yetu tutaona nyimbo na filamu nyingi zenye kuzingatia Mila na Desturi kuhakikisha watoto wanathaminiwa, wazee wanalindwa. Nyie kama kioo cha jamii mtuongoze ni wapi tunapaswa kwenda"amesema Dkt. Jingu.


Aidha Dkt Jingu ameongeza kuwa Ukatili unaotokea katika Jamii unasababishwa na mambo kadhaa, umaskini, mmomonyoko wa maadili hivyo kazi hili ni jukumu la wote ni kupambana na mmomonyoko wa maadili kwa ustawi wa jamii. 


Kwa upande wake Muasisi wa Tamasha hilo akiwakilisha mabalozi wa kupinga ukatili na msanii wa filamu Simon Mwapagata ameishukuru Serikali  kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum kwa kulifanyia kazi wazo la kuwa na Tamasha Hilo muhimu kwa lengo la kuifikia jamii katika ajenoya ukatili wa kijinsia na kulinda maadili ya mtanzania.


"Tumejipanga kwenda Mikoa, Wilaya Kata na Mitaa yote, kuanzia Kampeni hii ya Kupinga ukatili na kurudi maadili mema katika nchi hii, Tanzania sio chaka la kuletewa na kupokea kila kitu tuna mila na Desturi za kutuongoza. Tutaendelea kupambana kwa ajili ya kizazi chetu" amesema Mwapagata.



Naye Mwenyekiti wa Kampeni ya Shujaa wa Maendeleo na Ustawi wa Jamii (SMAUJATA) Taifa Sospeter Bulugu amesema anayo faraja kushiriki katika uzinduzi wa Tamasha la Fursa za Maendeleo kwa sababu litakuwa ni msaada katika kuendeleza juhudi za Mpango wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA) katika eneo la uchumi.


Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar Es Salaam Dkt. Rashid Mfaume akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Dar Es Salaam Mhe. Amos Makala ameahidi mkoa kuunga mkono maelekezo ya Serikali kupambana na ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto na kuongeza kwamba,  nguvu zaidi inahitajika kwa wadau kushirikiana na Serikali kama walivyojitokeza.


Tamasha hilo ni muendelezo wa kampeni ya Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wanawake na Makundi Maalum ya Twende Pamoja, Ukatili sasa basi na litafanyika katika mikoa yote kwa kuanza na mikoa ya Geita, Kagera, Mwanza, Mara, Kigoma, Songwe na Tanga, Rukwa na Tabora.


MWISHO


Tags

Chapisha Maoni

0Maoni
Chapisha Maoni (0)