Hayo yamesemwa tarehe 27 April 2023 Mkoani Dodoma na Naibu Waziri Wizara ya Uwekezaji Viwanda na Biashara Mhe. Exaud Kigahe (Mb) alipokutana na kufanya majadilino na wadau wa programu ya Maeneo Maalum ua Uzalishaji kwa mauzo ya nje (EPZ) na Programu ya kanda maalumu ya kiuchumi (SEZ).
Alisema Uwekezaji kupitia sekta binafsi una nafasi kubwa ya kuchangia utekelezaji wa malengo ya Kitaifa na kukuza sekta ya viwanda. Kukuza mauzo ya nje, kuzalisha ajira na kufundisha stadi za uzalishaji wa viwandani, kuendelea uhawilishaji wa teknologia ya Viwanda , kujenga uwezo wa kuzalisha bidhaa zinazoweza kuhimili ushindani wa masoko ya biashara kimataifa na uchakataji wa malighafi ili kuongeza thamani.
Aliongeza kusema juhudi kubwa zilizofanywa na Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuhamasisha Uwekezaji na kuvutia mitaji ya nje nchini na ndani ya nchi umeleta matokeo chanya mathalan katika miaka mitatu 2021-2023 kampuni 43 zilizosajiliwa katika mfumo wa EPZ zimeleta mtaji wa dola za Kimarekani milioni 134.29 na mauzo ya nje yenye thamani ya dola za Kimarekani milioni 134.39 na kuzalisha ajira za moja kwa moja 4,907 .
Kwa upande wake Muakilishi wa Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara Dkt. Yuda Lyangalo amesema Tanzania inawahitaji Wawekezaji hivyo kuwepo na majadiliano hayo ni fursa nzuri ya kuimarisha uhusiano.
Awali Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maeneo Maalumu ya Uwekezaji wa Mauzo ya Nje (EPZA) Bw. Charles Itembe alisema lengo la kikao hicho ni kusiliza hoja na changamoto mbalimbali za wawekezaji na Serikali kupitia Taasisi zake zilizoshiriki kikao hicho kutoa ufafanuzi wa masuala yanatakayoibuliwa.
Alisema mamlaka hiyo inaendelea kuendeleza na kusimamia maeneo hayo kwa kuweka miundombinu wezeshi na sera nzuri za kuvutia uwekezaji kwa kufikia malengo na maslahi mapana ya nchi.