Na.Alex Sonna-DODOMA
Mkuu wa Kitengo cha Mahusiano na Masoko Chuo cha Takwimu Mashariki Mwa Afrika, Eusebius Mwisongo amesema wamebuni mifumo itakayomsaidia mwananchi kufanya shughuli zake kiurahisi ili kuwa na mafanikio kwa haraka.
Hayo ameyasema leo Aprili 28,2023 jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye banda la Chuo hicho katika Maonesho ya wiki ya ubunifu 2023 yaliyoandaliwa na Wizara ya Elimu,Sayansi na Teknolojia yanayofanyika uwanja wa Jamhuri Dodoma.
Bw.Mwisongo amesema kuwa lengo ni kuujulisha umma umuhimu na faida za mifumo ya TEHAMA inayotengenezwa chuoni hapo.
“Tumekuja na mifumo sita ambayo inahusu ufatiliaji wa magari, mkulima, kufatilia mahudhulio ya wanafunzi na pamoja na mfumo wa vikoba”, amesema Mwisongo.
Ameitaja mifumo hiyo ni pamoja na E- Task Management,Vehicle Management System, e-mkulima,Class Tracking Attendance System, e-management.
Ameeleza kuwa Mifumo hiyo inafanya kazi tofauti kulingana na mahitaji ya mteja mfano kwa taasisi za elimu kuna mfumo wa class tracking attendance ambao huonyesha idadi ya wanafunzi walio hudhulia kipindi husika pamoja na mwalimu.
Lakini ameongeza kuwa wana mfumo wa e- task manengment ambao unawezesha mkuu wa kitengo kupanga majukumu kwa watu wake na wahusika hupata ujumbe wa majukumu waliopangiwa na kutekeleza majukumu yao na kuleta taarfa kupitia mfumo huo.
Hivyo ametoa wito kwa wananchi kutembelea banda lao hili kujua ni mafunzo gani wanatoa na huduma zinazopatikana katika banda lao hususani mifumo katika kuendesha shughuli za kijamii.

