Kazi za uwandani za urasimishaji makazi katika mitaa minne ya jiji la Dodoma zinatarajia kuanza rasmi Machi 6, 2023 baada ya kukamilika kwa kazi ya uhamasishaji wananchi ili kushiriki zoezi hilo.
Tayari zoezi la uhamasishaji limefanyika kwenye mitaa ya Mapinduzi A, Mapinduzi B katika Kata ya Ng’ong’ona, Mtaa wa Bihawana Kata ya Mbabala pamoja na Mtaa wa Mkwawa uliopo Kata ya Mpunguzi.
Hayo yamebainishwa na Meneja Mradi Urasimishaji Mjini, Bw. Leons Mwenda wakati wa zoezi la uhamasishaji wananchi kushiriki urasimishaji makazi katika Mtaa wa Mapinduzi B lililofanyika tarehe 1/3/2023 Jijini Dodoma.
Mwenda alisema, uhamasishaji ulifanyika katika ngazi ya Kitaifa, Halmashauri ya Jiji la Dodoma, kamati tatu za maendeleo ya Kata na sasa ni zamu ya wananchi katika ngazi ya mitaa lengo likiwa kuwapa uelewa wa pamoja wa kile kinachoenda kufanyika katika mitaa 4 ya jiji la Dodoma kupitia Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi.
‘‘Uhamasishaji umefanyika kwa mafanikio makubwa na katika mtaa huu wa Mapinduzi B zoezi la urasimishaji litaenda kuanza rasmi tarehe 6/3/2023 kwa kutambua, kupanga na kupima na mwisho mwananchi kupata hati miliki kwa mujibu wa Sheria ya Ardhi ya mwaka 1999’’ alisema Bw. Mwenda
Kwa mujibu wa Mwenda, zoezi hilo la urasimishaji litaenda kumuhusisha mwananchi moja kwa moja katika kila hatua ili kila mmoja awe na uhakika wa kile kinachofanyika ili kuepuka migongano isiyo ya lazima.
‘‘Urasimishaji ni mpango shirikishi wenye lengo la kutambua, kupanga, kupima na kumilikisha ardhi iliyojengwa bila kupangwa, na kauli mbiu ni tupange Miji yetu kwa pamoja ambapo kazi za uwandani zinatarajiwa kukamilika ndani ya miezi minne ili kutoa fursa ya wananchi kupatiwa hati miliki za ardhi yao’’ alisisitiza Bw. Mwenda
Naye Diwani wa Kata ya Ng’ong’ona Mhe. Loth H. Loth alisema kuwa, ardhi ndio uti wa mgongo wa wananchi hivyo mradi huu una manufaa kwa wananchi kwa kuwa ameufuatilia kwa karibu na kuona utekelezaji wake utakavyokuwa na kuwataka wananchi wa Mapinduzi B kuupokea mradi huo pamoja na kuwapa ushirikiano wataalamu watakaokwenda kutekeleza zoezi hilo.