Na Angela Msimbira, DAR ES SALAAM.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Angellah Kairuki ametoa siku saba kwa wataalamu wa Halmashauri ya Jiji la Dar es salaam kufanya tathmini ili kuangalia unafuu kwenye ujenzi wa shule katika maeneo yenye ufinyu wa ardhi.
Kauli hiyo ya Waziri Kairuki imekuja baada ya Mkuu wa Shule ya Msingi Kifuru jijini humo kuomba ridhaa ya kununua eneo lililopo pembezoni mwa shule hiyo au kubomoa majengo yaliyopo kwa ajili ya kujenga ghorofa ili kusaidia kupunguza msongamano kwa wanafunzi shuleni hapo.
Kutokana na ombi hilo, Waziri Kairuki amesema serikali itajenga shule mpya na kuitaka Halmashauri kuhakikisha eneo hilo linapatikana huku akiitaka kufanya tathmini ili kuangalia unafuu utakaosaidia kufanya maamuzi sahihi katika ujenzi wa shule hasa maeneo yenye ufinyu wa ardhi.
Akikagua miundombinu ya shule hiyo Leo Machi mosi, 2023 katika ziara yake ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika Kata ya Bunyoka jimbo la Segerea, amesema "Mkaangalie kipi kitatupa tija na ufanisi, kipi kitatupunguzia gharama, kipi kitatusaidia bila kufifisha taratibu na sera zetu za elimu na miongozo mbalimbali ya elimu nchini mimi ninachotaka shule nyingine ijengwe kwa ajili ya kupunguza msongamano wa wanafunzi.”
Amewataka wataalam hao kuhakikisha wanafanya tathmini ya kina itakayoonyesha kama Serikali itabomoa madarasa chakavu na kujenga ghorofa gharama zitakuwaje au kulipa fidia ili kutanua eneo husika kwa ajili ya kufanya ulinganifu.
Katika hatua nyingine, Waziri Kairuki amemuelekeza Kaimu Mkurugenzi wa Jiji hilo kuhakikisha anatumia mapato ya ndani kununua madawati 500, viti, meza za walimu 47, kujenga matundu ya vyoo 25 ya shule hiyo.